China imewawekea vikwazo waziri wa mawasiliano wa Paraguay, Gustavo Villate, na wa mambo ya nje wa Belize, Francis Fonseca, ikisema hatua hiyo inalenga kuwaadhibu na pia kutoa onyo kwa viongozi wengine.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, Mao Ning, amesema baadhi ya wanasiasa wa Paraguay na Belize wamekubali kutumiwa na mamlaka za Taiwan katika juhudi zake za kutafuta kile Beijing inachokiita uhuru kwa msaada wa mataifa ya nje.
Kwa mujibu wa China, vikwazo hivyo vinahusisha kufungiwa mali zao nchini humo, kunyimwa visa za kuingia China na kupigwa marufuku kwa mashirika ya China kufanya biashara nao.
China imesema mawaziri hao wamechukua hatua na kutoa matamshi ambayo yameharibu maslahi ya msingi ya taifa hilo.
Beijing pia imeeleza kuwa hatua hizo zimechukuliwa kwa lengo la kulinda usalama wa taifa na kupinga shughuli za kujitenga.
Taiwan haijatoa tamko rasmi kuhusu vikwazo hivyo dhidi ya viongozi hao wa Amerika ya Kusini.


