Mheshimiwa Rais,

Mwaka 1980, nikiwa bado mtoto mdogo kabisa, nilishiriki gwaride la uzimaji wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa kijijini Butiama. Wakati wa ushonaji wa sare za chipukizi, vipimo vyangu vilichukuliwa kuwakilisha ushonaji wa nguo za chipukizi wenye miili midogo!

Hiyo ni miongoni mwa kumbukumbu za maisha yangu ambazo nimeendelea kuwa nazo. Nilikuwa mtoto, lakini nilikuwa sehemu ya historia ya taifa lililokuwa likijenga utambulisho, likijivunia uhuru wake na kuamini kuwa Mwenge wa Uhuru ungeendelea kuwaongoza Watanzania katika safari ya maendeleo, umoja, upendo na utu.

Kuna wimbo maarufu wa Mwenge unaotokana na maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyoyatoa wakati taifa letu likijiandaa kupata uhuru kutoka kwa Waingereza. Mwalimu alisema:

“Tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu; ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini; upendo mahali palipo na chuki; na heshima palipojaa dharau.”

Maneno haya ni ahadi ambayo taifa letu lilijiwekea. Ni kipimo cha namna tunavyopaswa kuishi, kutawala, kuheshimiana na kutatua tofauti zetu. Ni mwongozo unaopaswa kutukumbusha kuwa uhuru haupaswi kuwa bendera na mipaka pekee, bali pia ni dhamana ya kulinda utu, haki na uhai wa kila Mtanzania.

Mheshimiwa Rais, naandika makala hii moja kwa moja kwako kwa imani kuwa utaisoma wewe mwenyewe. Kwa bahati mbaya, tumekuwa na jamii ya wapika majungu waliokubuhu. Sisi tunaojitahidi kuwa wakweli kwa nia nzuri ya kulitakia heri taifa letu, tunapigwa ‘shoti’ ili tuonekane hatuna uzalendo au tunatumiwa na mabeberu.

Katika kitabu cha Wagalatia 4:16 kuna maneno haya: “Je, nimekuwa adui yenu kwa sababu nawaambia yaliyo kweli?”

Mtume Paulo anauliza swali hili baada ya kuzungumzia uhusiano wake na Wagalatia. Aya hii inaonyesha changamoto ambayo watu wanaosema ukweli wanaweza kukutana nayo. Badala ya kusikilizwa, wanaweza kuchukiwa kwa sababu ya ujumbe wao. Naomba uwapuuze. Tunakusaidia kwa kukueleza wasiyokueleza.

Ndugu Rais, Oktoba hii, sura ya Tanzania katika miji na vijiji imepambwa kwa majonzi na kumbukumbu ya siku iliyobadilisha taswira ya taifa letu daima.

Mwaka mmoja uliopita, ardhi ya nchi yetu iliyosifika kwa miongo mingi kama kisiwa cha amani ililowa damu ya raia wake wasio na hatia. Oktoba 29, 2025, iligeuka kuwa alama ya giza totoro, kilio cha kusaga meno na jeraha linaloendelea kuumiza utaifa wetu.

Siku hiyo ilianza kama siku nyingine ya kawaida, lakini haraka mno iligeuka kuwa uwanja wa maangamizi. Milio ya risasi za moto, vilio vya watu waliokuwa wakikimbia ovyo kuokoa maisha yao na moshi mzito wa gesi ya machozi viliteka miji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Mara na maeneo mengine nchini.

Raia waliokuwa mitaani, wafanyabiashara wadogo, watoto, kina mama na wazee walijikuta katikati ya hali isiyoelezeka. Wengi walikuwa watu wa kawaida waliokuwa wakitafuta riziki, wakitekeleza shughuli zao za kila siku na kuishi katika nchi waliyoamini kuwa ni salama kwao.

Maiti zilitapakaa barabarani na mitaani mithili ya majani yaliyopukutika wakati wa kiangazi. Mamia ya watu walipoteza maisha siku hiyo na katika siku zilizofuata, wengi wao wakiwa vijana wenye ndoto kubwa na Watanzania waliokuwa wakihangaikia mkate wa kila siku kwa ajili ya familia zao.

Mbali na vifo hivyo, maelfu ya Watanzania walibaki na ulemavu wa kudumu wa miili na akili. Wapo waliopoteza viungo vyao na sasa wanatumia viti vya magurudumu; wapo waliopoteza uwezo wa kuona; na wengine wanaendelea kuishi na vipande vya risasi miilini mwao. Zaidi ya hayo, kovu la kisaikolojia limebaki donda ndugu kwa mashuhuda wengi ambao bado wanaishi na jinamizi la kuona wapendwa wao wakikata roho.

Haya yalienda sambamba na maangamizi makubwa ya kiuchumi. Maduka na vituo vya mafuta vilichomwa moto, magari yaliteketezwa na mifumo ya biashara iliyochukua miongo kadhaa kuijenga iligeuka majivu ndani ya saa chache. Familia zilizokuwa zikijitegemea zilitumbukia kwenye umaskini uliokithiri.

Mheshimiwa Rais, maafa haya hayawezi kuangaliwa kama tukio la siku moja lililopita na kuachwa katika vitabu vya historia. Ni maumivu yanayoendelea kuishi katika familia zilizopoteza wapendwa wao, kwa majeruhi wanaoishi na athari za kudumu, kwa watu waliopoteza mali zao na kwa taifa letu. Tumejikuta tukijiuliza maswali mazito kuhusu mustakabali wa amani na mshikamano wetu.

Kutokana na maafa hayo makubwa, iliundwa Tume ya Uchunguzi chini ya Jaji Mstaafu Mohamed Chande ili kufichua mizizi ya kadhia hiyo. Ripoti hiyo iliweka mbele ya taifa hoja na masuala yanayohitaji kutazamwa kwa uzito, ikiwamo migogoro ya muda mrefu ambayo haikupata ufumbuzi wa kuridhisha.

Kwa mujibu wa Tume ya Jaji Chande, chanzo kikuu cha mlipuko huo kilikuwa mgogoro wa kidemokrasia na kukosekana kwa haki, kulikotokana na kufungwa kwa milango ya uhuru wa kiraia, michakato ya uchaguzi isiyoaminika na hisia za wananchi kwamba sauti zao hazina tena thamani.

Tume ilieleza pia kuhusu kuporomoka kwa imani ya umma kwa taasisi muhimu kama Tume ya Uchaguzi, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mahakama na Jeshi la Polisi, ambazo kwa mtazamo wa wananchi zilionekana kuegemea upande mmoja badala ya kusimamia Katiba na haki.

Tume ilibainisha pia kuwa hali ngumu ya kiuchumi, kupanda kwa gharama za maisha na ukosefu wa ajira miongoni mwa mamilioni ya vijana vilijenga hasira kubwa iliyokuwa ikisubiri cheche ndogo tu ili kulipuka.

Hali hiyo ilichochewa zaidi na matumizi ya lugha kutoka kwa baadhi ya wanasiasa wa pande zote, sambamba na mengine yaliyosambazwa mitandaoni. Aidha, matumizi ya nguvu yaliyopitiliza dhidi ya raia yalitajwa kuwa miongoni mwa masuala mazito yanayohitaji uwajibikaji na mageuzi ya namna vyombo vya dola vinavyotekeleza dhima yake ya kulinda wananchi.

Mheshimiwa Rais, kutambua sababu za maafa si kutafuta mtu wa kumlaumu. Ni kutafuta ukweli ili kuhakikisha kuwa kilichotokea hakijirudii. Taifa haliwezi kujenga mustakabali salama kwa kuficha majeraha yake; haliwezi kurejesha imani kwa kukwepa maswali magumu; na haliwezi kuimarisha umoja kwa kutaka waathirika wasahau kabla hawajapata haki. Baba wa Taifa alisema, “Hatuwezi kuondoa matatizo yetu kwa kujidanganya kuwa hayapo.”

Wakati matukio hayo yakitokea, hali ilikuwa ya kutisha mno. Tanzania ilitawaliwa na amri za kutotoka nje, mawasiliano ya intaneti yakazimwa, hofu ikatawala kila nyumba, na jumuiya ya kimataifa ikatutazama kwa mshangao huku shughuli za kiuchumi na utalii zikipata athari kubwa.

Mwaka mmoja baadaye, tujiulize kama imani ya wananchi kwa dola, taasisi za umma na mifumo ya haki imeanza kurejea. Je, familia zilizoathirika zimepata msaada unaostahili? Waliopoteza wapendwa wao wamepata majibu? Je, vijana wanaamini kuwa wanaweza kutofautiana na viongozi wao bila kuhatarisha maisha yao? Utekaji umekoma?

Mheshimiwa Rais, iwapo taifa linataka kurejea katika hali ya utulivu wa kudumu, hatuna budi kuyatafakari na kuyafanyia kazi mapendekezo ya Tume ya Jaji Chande; na kwa kweli, hiyo ndiyo maana mojawapo ya kuundwa kwa tume hiyo.

Umoja wetu umetikiswa na chuki na kutoaminiana kati ya watawala na watawaliwa. Iwapo tutakubali ukweli, tukatubu pale tulipokosea na kufanya mabadiliko ya kina, maumivu ya siku hiyo yanaweza kuwa chachu ya kuzaliwa upya kwa Jamhuri inayoheshimu utu na sheria.

Kwa heshima kubwa, ninakuomba, kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uongoze mchakato wa kitaifa wa kutafuta ukweli, kurejesha imani na kuponya majeraha ya Oktoba 29, 2025. Ninaamini kuwa hatua zifuatazo zinastahili kupewa kipaumbele:

Kwanza, kutekeleza mapendekezo ya Tume kwa uwazi na kwa ratiba inayoeleweka. Serikali iweke bayana mapendekezo yatakayotekelezwa, hatua zilizochukuliwa, muda wa utekelezaji na namna wananchi watakavyopima maendeleo yake. Haya yanawezekana hata bila kusubiri ripoti ya Tume ya Jaji Lila. Pale ambapo mapendekezo yanahitaji hatua za kisheria au mabadiliko ya kitaasisi, hatua hizo zichukuliwe bila kigugumizi.

Pili, kuhakikisha uwajibikaji wa kisheria baada ya ripoti ya Jaji Lila. Yeyote atakayebainika kuwa aliamuru, alitekeleza au alihusika katika uhalifu unaohusiana na vifo, majeraha na ukiukwaji wa haki za wananchi anapaswa kuchunguzwa na, pale ushahidi unapotosha, kufikishwa katika vyombo vya sheria bila kujali cheo, nafasi au mamlaka yake. Uwajibikaji huo sharti ufuate sheria, ushahidi, haki ya kusikilizwa na uhuru wa mahakama.

Tatu, kilio cha umma ni mabadiliko ambayo, kwa bahati nzuri, uliyaasisi wewe mwenyewe. Anzisha mageuzi ya kikatiba na ya taasisi za kidemokrasia. Mageuzi yanapaswa kujenga mifumo imara ya uwajibikaji, kulinda uhuru wa taasisi na kuimarisha imani ya wananchi katika michakato ya uchaguzi, Mahakama, Jeshi la Polisi na taasisi nyingine za umma. Katiba na sheria vinapaswa kuwa kinga ya raia dhidi ya matumizi mabaya ya mamlaka.

Nne, nakuomba ufanye mageuzi ya kimtazamo na kikanuni katika vyombo vya dola. Polisi na vyombo vingine vya usalama vinapaswa kutambua kuwa dhima yao ya msingi ni kulinda maisha, usalama na haki za wananchi kwa mujibu wa Katiba na sheria. Matumizi ya nguvu lazima yawe ya lazima, ya uwiano na ya mwisho pale njia nyingine salama zinaposhindwa. Matumizi ya nguvu yaliyopitiliza dhidi ya raia hayapaswi kuwa sehemu ya namna ya kawaida ya kusimamia mikusanyiko au kutatua tofauti za kisiasa. Juzi tumeona vurugu za Ufaransa. Hakuna watu 500 waliouawa!

Naomba uwekwe mpango wa kuwasaidia waathirika na familia zilizoathirika. Waliopoteza wapendwa wao, waliojeruhiwa, waliopata ulemavu na waliopoteza mali wanahitaji utaratibu wa wazi wa kupokea msaada, matibabu, huduma za kisaikolojia na, pale inapothibitishwa kuwa inastahili, fidia kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Rais, tujenge utamaduni wa mazungumzo na maridhiano ya kitaifa. Maridhiano hayawezi kuwa agizo tu la kusahau yaliyotokea. Yanahitaji ukweli, kusikilizana, kukubali maumivu ya wengine na kujenga mazingira ambayo tofauti za kisiasa hazitafsiriwi kama uadui dhidi ya taifa.

Waathirika, familia zao, vijana, asasi za kiraia, viongozi wa dini, vyama vya siasa na makundi mengine ya wananchi wanapaswa kupata nafasi ya kushiriki katika mchakato huo.

Mheshimiwa Rais, wajibu wa kulinda taifa si wa Serikali pekee. Sisi wananchi tuna wajibu mzito wa kulinda taifa letu kwa kukataa kugawanywa kwa misingi ya kisiasa, kikabila au kidini.

Nauasa umma uendelee kudai haki na uwajibikaji kwa njia za kistaarabu na amani, ukiepuka mitego ya ghasia na uharibifu wa mali, huku ukisimama kidete kupaza sauti pale misingi ya utu inapovunjwa. Wanasiasa nao wana wajibu wa kukataa lugha za chuki, uchochezi na siasa zinazowafanya Watanzania waone wenzao kama maadui.

Hata hivyo, wajibu wa wananchi kudumisha amani haupaswi kutumiwa kama sababu ya kuwanyima uhuru wa kueleza malalamiko yao au kudai haki. Amani na haki ni vitu vinavyotegemeana. Taifa linalolinda amani kwa kuzuia sauti za malalamiko na ukosoaji linaweza kuonekana limetulia kwa nje, lakini likawa linaendelea kubeba hatari kubwa ndani yake.

Mheshimiwa Rais, ninaporejea kumbukumbu yangu ya mwaka 1980, nikiwa mtoto mdogo katika gwaride la uzimaji wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa kijijini Butiama, ninajiuliza: Je, mwanga wa Mwenge tunaouendeleza leo unaangaza vya kutosha pale ambako kuna majonzi, chuki, dharau na kukosekana kwa matumaini?

Mwalimu Nyerere alitamani Mwenge umulike hata nje ya mipaka yetu; ulete tumaini pale ambako hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau. Hiyo ndiyo Tanzania ambayo vizazi vilivyotutangulia vilitaka kuijenga, na ndiyo Tanzania tunayopaswa kuiachia vizazi vijavyo.

Tunapowasha mishumaa ya kumbukumbu mwaka mmoja baada ya janga hili, msimamo wetu Watanzania wote uwe wa kuapa kuwa kamwe damu ya Watanzania isije ikamwagika tena kwa sababu ya tofauti za kisiasa au hofu ya mabadiliko kama ilivyotokea mwaka 2025.

Hata hivyo, Tanzania itakuwa salama endapo tu sote—watawala na watawaliwa—tutaweka kando tofauti na ubinafsi na kuiona nchi hii kuwa mali yetu sote.

Njia pekee ya kuwapa heshima wote waliouawa au kuumizwa Oktoba 29, 2025, ni kujenga taifa ambalo haki inatawala, uhuru unalindwa na kila uhai wa mwanadamu unaonekana kuwa wa thamani.

Mheshimiwa Rais, historia itatupima kwa namna tulivyowatendea wananchi wakati wa kutokubaliana, kwa jinsi tulivyowajibika baada ya maafa na kwa hatua tulizochukua kuzuia maafa kama hayo yasijirudie.

Mwenge wa Uhuru haupaswi kuwa mwanga wa sherehe pekee. Unapaswa kuwa mwanga wa dhamiri ya taifa. Na mwanga huo utakuwa na maana ya kweli pale ambapo kila Mtanzania ataweza kuishi bila hofu, kudai haki kwa amani na kutambua kuwa maisha yake yana thamani sawa mbele ya sheria. Wananchi wananung’unika. Taifa linahitaji kuponywa.

Mheshimiwa Rais, kama nilivyosema awali, nimeandika waraka huu ukiwa ni mchango wangu kwa taifa letu ambalo mimi ni miongoni mwa wale tunaolipenda mno.

Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Jamhuri yetu. Mungu atujalie ujasiri wa kukabili ukweli, kutenda haki na kujenga upya umoja wetu.

Kwa heshima,

Manyerere Jackton

0759 488955