• Wadai kuahidiwa fidia ya Sh 4,700 kwa mita moja ya mraba, tathmini zaonyesha Sh 500 hadi 1,300
Na Pendo Nguka, JamhuriMedia, Serengeti
Malalamiko ya fidia yameibuka miongoni mwa zaidi ya kaya 140 zinazotarajiwa kupisha mradi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Serengeti mkoani Mara, huku wananchi wakidai tofauti kubwa kati ya bei waliyoelezwa awali na viwango vilivyojitokeza kwenye nyaraka za uthamini.
Wakazi wa Morotonga, Burunga na Kyambahi wanasema katika mkutano wa Aprili 13, 2026 walielezwa kuwa fidia ya ardhi ingekuwa Sh 4,700 kwa mita ya mraba, lakini nyaraka za tathmini walizopokea zinaonyesha viwango vya Sh 500 hadi Sh 1,300.
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Serengeti unaotekelezwa na serikali unatarajiwa kupunguza muda wa wageni kufika kwenye Hifadhi ya Taifa Serengeti (SENAPA).
Mbali na tofauti zilizojitokeza kwenye fidia, wananchi wanahoji kwa nini wamiliki wenye mashamba yanayofanana kwa ukubwa wanapangiwa jumla ya fidia zisizolingana na hesabu wanazofanya kwa viwango walivyoelezwa? Wanataka kujua maeneo yaliyopimwa, bei iliyotumika na thamani ya mali nyingine zilizojumuishwa.
Wananchi wanasisitiza kwamba hawaipingi miradi ya maendeleo, lakini wanaogopa kuondolewa kwenye ardhi waliyoitumia kwa makazi, kilimo na ufugaji kwa miongo kadhaa bila fedha zinazowawezesha kuanza maisha mapya.
Kwao, tofauti ya Sh 4,700 waliyosema kuahidiwa na Sh 600 inayojitokeza kwenye baadhi ya tathmini ni zaidi ya Sh 4,000 kwa mita ya mraba. Kwa ekari moja, tofauti hiyo inaweza kufikia takribani Sh milioni 16.59.
Hiyo ndiyo sababu wanataka rekodi za mikutano, fomu za uthamini na vigezo vya bei vitolewe hadharani. Hata hivyo, kiwango cha Sh 4,700 bado ni madai ya wananchi yanayohitaji kuthibitishwa na mamlaka zilizoshiriki mkutano huo.
KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA OKTOBA 27


