*EWURA, NEMC zakiri kutoa vibali; wananchi wahoji usiri wa kugawa maeneo ya hifadhi
NA Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Usiri kuhusu ujenzi ndani ya Hifadhi ya Barabara ya Morogoro umeendelea kutikisa, huku baadhi ya kanuni za ujenzi wa vituo vya mafuta zikidaiwa kukiukwa.
Miongoni mwa kanuni hizo ni ya kutoa muda wa kutosha, au kutokuwapo kabisa matangazo ya awali kabla ya ujenzi ya kupata maoni ya wananchi kuhusu eneo au maeneo yanayokusudiwa kujengwa vituo vya mafuta.
Ukaribu wa vituo hivyo ni jambo jingine lililoibuka kwenye malalamiko ya baadhi ya wananchi, wakisema ujenzi unaoendelea unaonekana kupuuza kanuni ya umbali kati ya kituo na kituo.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) zimekiri kutoa vibali kwa wawekezaji wanaojenga vituo vya mafuta katika maeneo ya hifadhi ya Barabara ya Morogoro, huku maswali yakiendelea kuhusu masharti ya matumizi ya ardhi hizo na uhalali wa ujenzi unaoendelea.
Taarifa hizo zimekuja wakati ujenzi wa vituo kadhaa vya mafuta ukiendelea kwa kasi katika maeneo ya kuanzia Kimara hadi Kibaha Maili Moja mkoani Pwani, hali inayozua maswali kuhusu namna mamlaka zinavyoratibu matumizi ya hifadhi ya barabara na kuhakikisha masharti ya vibali yanafuatwa.
Suala jingine linalohitaji ufafanuzi ni ukaribu wa vituo kadhaa vya mafuta vinavyojengwa eneo la Temboni. Baadhi ya wadau wamehoji iwapo vibali vya ujenzi vilizingatia umbali kati ya kituo kimoja na kingine, pamoja na masharti ya mipango miji na usanifu wa barabara.
Wakati kanuni za ujenzi wa vituo vya mafuta zikitaka umbali wa kituo kimoja na kingine kwa upande mmoja uwe meta zisizopungua 200, hali ni tofauti kwa eneo la Barabara ya Morogoro, mfano halisi ukiwa Temboni. Katika eneo hilo, kunajengwa vituo vitatu ndani ya eneo ambalo kukitokea janga la moto huenda ukasababisha janga kubwa kwa vituo na watumiaji wengine wa barabara.
Aidha, miundombinu inayojengwa hapo haionyeshi dalili ya kwamba si ya kudumu, bali ni uwekezaji mkubwa unaogharimu mamilioni kama si mabilioni ya shilingi.
Meneja wa EWURA, Kanda ya Mashariki, Lorivii Long’indu, amesema mamlaka hiyo hutoa vibali vya ujenzi baada ya waombaji kutimiza masharti yanayotakiwa, ikiwamo kupata nyaraka za matumizi ya ardhi, tathmini ya mazingira na kibali cha ujenzi kutoka mamlaka za serikali za mitaa.
Long’indu anasema EWURA huingia katika mchakato baada ya taasisi nyingine zinazohusika na matumizi ya ardhi na mazingira kukamilisha sehemu zao za kazi.


