Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mtwara
Mtanzania anayefanya biashara ndogo sokoni, mkulima wa kijijini, dereva wa bodaboda au mama lishe sasa ana fursa ya kupata bima ya afya kwa ajili yake na familia, bila kulazimika kuwa mtumishi wa serikali au wa kampuni kubwa; JAMHURI linaripoti.
Ujumbe huu unaotia matumaini umetolewa wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, Oktoba 22, 2026, katika Uwanja wa Sabasaba mkoani Mtwara, huku shughuli nyingine kama hizo zikiendeshwa katika mikoa mbalimbali nchini.
Awamu hii inalenga kusajili kaya 625,000, ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi, hasa wale wanaotegemea kipato cha kila siku.
Akizindua mpango huo kwa niaba ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amesema dhamira ni kuhakikisha ugonjwa hauwi sababu ya familia kuuza mali au kushindwa kupata matibabu.
“Bima ya Afya kwa Wote haimaanishi kwamba kila mwananchi atapata bima bure. Hapana! Kisima hakichimbwi na mtu mmoja. Mwananchi mwenye uwezo atachangia bima yake na ya familia yake, kulingana na utaratibu uliowekwa,” amesema Mchengerwa.
Sh 150,000 inalinda nani?
Katika hatua inayogusa maisha ya wananchi wengi, Serikali imeanzisha kifurushi cha ‘Fahari Afya’, kinachogharimu Sh 150,000 kwa mwaka kwa kaya yenye watu wasiozidi sita.
Kaya hiyo inaweza kujumuisha mkuu wa kaya, mwenza wake na wategemezi wasiozidi wanne.
Wategemezi wanaoruhusiwa ni pamoja na watoto wa kuzaa, kuasili au wa kambo walio chini ya miaka 21, wazazi wa mwanachama au mwenza wake, pamoja na ndugu wa damu wanaokidhi masharti.
Mtu asiye na mwenza au watoto pia anaweza kujiunga kama kaya ya mtu mmoja. Familia yenye watu zaidi ya sita inaweza kuunda kaya nyingine kwa utaratibu uliowekwa.
Akizungumzia gharama za bima, Mchengerwa amelinganisha uchaguzi wa vifurushi vyake na vifurushi vya simu.
“Vifurushi si jambo geni! Hata kwenye simu zenu kuna vifurushi vya siku, vya wiki, vya mwezi; kweli au si kweli? Unachagua kifurushi kulingana na fedha uliyonayo. Na katika bima ya afya utaratibu ni huo huo! Unachagua kifurushi kulingana na uwezo wako wa kuchangia,” amesema.
Mbali na NHIF, wananchi wanaweza kupata bima kupitia kampuni binafsi zilizoidhinishwa, chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA).
KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA OKTOBA 27- NOVEMBA 2, 2026



