*Akemea ubadhirifu wa fedha za maendeleo, mauaji yanayotokana na migogoro ya mapenzi

Na Kulwa Karedia, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, Michael Msonganzila, amewataka wasimamizi wa miradi ya maendeleo kuacha wizi na kuhakikisha fedha zinazotengwa na serikali zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Amesema vitendo vya ubadhirifu vinachelewesha utekelezaji wa miradi, vinadhoofisha ubora wa miundombinu na kuwarudisha nyuma wananchi wanaotarajia kupata huduma bora.

Akizungumza katika mahubiri ya Jumapili mjini Musoma, mkoani Mara, mwishoni mwa wiki, Askofu Msonganzila amesema serikali inatekeleza miradi mingi ya shule, barabara na huduma za afya, lakini baadhi ya watu wanaokabidhiwa kuisimamia wanatumia nafasi zao kujinufaisha.

“Tunajua serikali inafanya mambo mengi mno, inatengeneza miundombinu, shule, itatutengenezea barabara. Haya yote ni majukumu ya lazima kwa ustawi wa watu wake, lakini katika kutengeneza miundombinu watu wengine wanaiba fedha,” amesema.

Ametoa mfano wa barabara inayotengenezwa kwa Sh bilioni 100 lakini, kwa madai yake, hujengwa kwa Sh bilioni 50, huku kiasi kilichobaki kikigawanywa kwa watu wenye vyeo.

“Huu ni wizi mbaya ambao unarudisha nyuma maendeleo. Tunataka kuona kiasi chote kinachotengwa kinakwenda barabarani ili tuone kama tutapata barabara mbaya kila baada ya miezi mitatu,” amesema.

Amesema matumizi sahihi ya fedha za umma yangesaidia kupunguza tatizo la barabara kuharibika muda mfupi baada ya kujengwa na kuboresha huduma nyingine muhimu.

Akizungumza na waumini waliokuwa wakipokea Sakramenti ya Kipaimara, amewakumbusha kwamba baadhi yao watakuwa viongozi, wahandisi na madaktari, hivyo wanapaswa kuishi kwa uaminifu katika majukumu yao.

“Ninyi waamini mnaopata Kipaimara leo, ninyi ndio wahusika. Mmekuwa wahandisi, mmekuwa marais, mmekuwa madaktari; dawa zinakuja kwenye vituo vya afya, mnazichepusha,” amesema.

Amewataka waumini kuzingatia amri ya Mungu inayokataza wizi na kujenga jamii inayothamini haki, amani, upendo, upatanisho na uvumilivu.

Amesisitiza kwamba uaminifu unapaswa kuanzia kwa mtu binafsi, huku kila mmoja akitambua wajibu wake wa kulinda mali ya umma na kutenda haki.

Kwa upande wa miradi, ujumbe wa Askofu Msonganzila unalenga kuwafanya wenye dhamana kutambua kuwa fedha zinazotolewa kwa ajili ya maendeleo zinapaswa kuwanufaisha wananchi. Amesema kujenga barabara zisizodumu au kuchepusha vifaa na fedha kunawanyima wananchi huduma wanazozihitaji. Kwa upande wa mahusiano, amesisitiza kuwa hasira na wivu havipaswi kutumiwa kuhalalisha ukatili, huku akiwahimiza wazazi na walezi kuwasaidia vijana kujenga tabia ya kuvumiliana na kusikilizana kabla migogoro haijageuka kuwa madhara.

KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA OKTOBA 27 – NOVEMBA 2, 20206