Na Stella Aron, JamhuriMedia, Dodoma
UTABIRI wa mvua nyingi unaotokana na kuimarika kwa hali ya El Niño umeibua tahadhari mpya kuhusu usalama wa chakula, maisha ya wananchi na miundombinu nchini, huku Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ikizitaka sekta mbalimbali kujiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza katika msimu wa mvua wa mwaka 2026/2027.
Hali hiyo inatarajiwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na ongezeko la joto la maji katika eneo la tropiki ya kati ya Bahari ya Pasifiki, linalohusishwa na hali ya El Niño yenye nguvu kubwa, pamoja na mifumo mingine ya bahari na upepo inayoweza kuimarisha mvua katika baadhi ya maeneo nchini.
Akizungumza wakati wa kutangaza utabiri wa msimu huo Oktoba 23, 2026,Ladislaus Benedict Chang’a ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO anasema mvua nyingi zaidi zinatarajiwa katika kipindi cha Novemba 2026 hadi Januari 2027, huku kiwango cha mvua kikitarajiwa kupungua kuanzia Februari hadi Aprili 2027.
Chang’a ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (Intergovernmental Panel on Climate Change-IPCC) anasema kuwa utabiri huo, mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe na Rukwa, pamoja na maeneo ya kusini mwa Morogoro, inatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani hadi wastani.Mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Hata hivyo, changamoto kubwa si kiasi cha mvua pekee, bali pia muda wa kunyesha, usambazaji wake na namna jamii zilivyojiandaa kukabiliana na athari zake.
TMA imeeleza kuwa mvua zitaanza kuenea katika maeneo mengi nchini mwezi Novemba, ingawa baadhi ya maeneo ya Tabora, Katavi, Kigoma, Lindi na Mtwara yanatarajiwa kuanza kupata mvua hizo kuanzia wiki ya nne ya Oktoba hadi wiki ya kwanza ya Novemba.
Mvua hizo zinatarajiwa kukoma katika maeneo mengi kati ya wiki ya tatu na ya nne ya Aprili 2027, huku maeneo ya magharibi na Nyanda za Juu Kusini Magharibi yakitarajiwa kuendelea kupata mvua hadi wiki ya kwanza ya Mei.
Mifumo ya bahari na upepo kuchochea mvua.
Akifafanua sababu zinazoweza kuimarisha mvua hizo, Dkt. Chang’a anasema mifumo ya bahari na upepo inatarajiwa kuchangia ongezeko la mvua, ikiwemo upepo wenye unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo kuelekea maeneo ya magharibi na Kanda ya Kati.
Anasema pia joto la maji katika eneo la magharibi mwa Bahari ya Hindi linatarajiwa kuwa juu ya wastani ikilinganishwa na eneo la mashariki, hasa katika nusu ya kwanza ya msimu, hali inayoweza kuimarisha mifumo ya mvua nchini.
Kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, yakiwemo Ukanda wa Ziwa Victoria, Kaskazini mwa nchi na Ukanda wa Pwani, mvua za Vuli zimeanza kunyesha katika baadhi ya maeneo kama ilivyotabiriwa.
Ongezeko la mvua hizo linatarajiwa Novemba na Desemba 2026, huku mvua za nje ya msimu zikitarajiwa kuendelea Januari 2027.

KILIMO NA USALAMA WA CHAKULA HATARINI
Sekta ya kilimo, ambayo ni tegemeo la maisha ya wananchi wengi nchini, ni miongoni mwa maeneo yanayoweza kuathiriwa na mvua nyingi zinazotarajiwa.
Kwa mujibu wa TMA, mvua hizo zinaweza kusababisha maji kutuama mashambani, mafuriko na kuongezeka kwa unyevunyevu kwenye udongo, hali inayoweza kuathiri ukuaji wa mazao na kuharibu miundombinu ya kilimo.
Mazingira hayo pia yanaweza kuongeza magonjwa ya mazao yanayosababishwa na fangasi, bakteria na virusi, na kuathiri uzalishaji wa viazi mviringo, alizeti, maharage, ufuta, matunda na mbogamboga.
Athari nyingine ni kuvurugika kwa shughuli za uvunaji, ukaushaji, usafirishaji na uhifadhi wa mazao, jambo linaloweza kuongeza upotevu wa chakula baada ya kuvuna.
Hali hiyo inaonesha umuhimu wa wakulima kutotegemea mvua kama chanzo pekee cha mafanikio ya kilimo, bali pia kuzingatia taarifa za hali ya hewa katika kupanga muda wa kupanda, kuchagua mbegu na kusimamia mashamba yao.
TMA imewashauri wakulima kuandaa mashamba mapema, kupanda kwa wakati, kutumia mbegu zinazofaa kwa mazingira yao na kuzingatia ushauri wa maafisa ugani. Pia wametakiwa kuweka mifereji ya maji, kutumia matuta na mbinu za kilimo cha kontua ili kupunguza kutuama kwa maji, mmomonyoko wa udongo na upotevu wa rutuba.
Kwa wafugaji, mvua hizo zinatarajiwa kuongeza upatikanaji wa malisho na maji kwa mifugo. Hata hivyo, TMA imeonya kuwa unyevunyevu mwingi unaweza kuongeza hatari ya magonjwa, yakiwemo homa ya bonde la ufa na kuoza kwa kwato.
Miundombinu, afya na usafiri kuathirika
Mbali na kilimo, mvua nyingi zinaweza kuwa na athari katika sekta za usafiri, afya, ujenzi na uchimbaji madini.
Dkt. Chang’a anasema ongezeko la maji katika mito na mabwawa linaweza kuambatana na uchafuzi wa vyanzo vya maji, hali inayoweza kuongeza hatari ya magonjwa ya mlipuko.
Katika sekta ya usafiri, athari zinazoweza kujitokeza ni pamoja na kuharibika kwa barabara, kuporomoka kwa kingo, kuharibika kwa madaraja na njia za reli, pamoja na kuchelewa kwa huduma za usafiri wa anga na majini.
Mvua kubwa zinazoambatana na radi na upepo mkali zinaweza pia kupunguza uono kwa marubani na kuathiri ratiba za safari za ndege.
Kwa upande wa sekta ya ujenzi, mvua zinaweza kuchelewesha utekelezaji wa miradi, kuongeza gharama, kuharibu vifaa na kuhatarisha usalama wa wafanyakazi pamoja na watumiaji wa miundombinu.
TMA imewashauri wakandarasi kuzingatia utabiri wa hali ya hewa wanapopanga shughuli zao, kuhamisha mitambo kutoka maeneo ya mabonde na chemchemi na kuhifadhi vifaa vinavyoweza kuharibika vikilowa, ikiwemo saruji, katika sehemu salama.
Katika shughuli za uchimbaji madini, hasa migodi midogo, mvua nyingi zinaweza kuongeza hatari ya maporomoko ya ardhi na kuporomoka kwa mashimo yasiyo imara.

SERIKALI NA WANANCHI WASHAURI KUJIANDAA
Kutokana na athari zinazoweza kujitokeza, TMA imezitaka mamlaka za serikali za mitaa kuimarisha mifumo ya mifereji ya maji, kutoa elimu kwa wananchi na kuimarisha kamati za maafa katika ngazi za mikoa, wilaya, kata, vijiji na mitaa.
Katika sekta ya afya, imeshauri kuimarishwa kwa udhibiti wa mazalia ya mbu, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, pamoja na kuandaliwa kwa mipango mbadala ya kuendelea kutoa huduma za afya endapo miundombinu ya usafiri itaharibika.
Aidha, mvua hizo zinaweza kuathiri wanyamapori na shughuli za utalii, huku baadhi ya wanyama wakihamia katika makazi ya watu na kuongeza uwezekano wa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Dkt. Chang’a amewataka wananchi na wadau wa sekta mbalimbali kuendelea kufuatilia utabiri wa hali ya hewa wa kila siku, siku 10 na kila mwezi ili kupanga shughuli zao kwa kuzingatia mwenendo wa hali ya hewa katika maeneo yao.
Kwa hali hiyo, utabiri wa mvua za msimu wa 2026/2027 unatoa ujumbe muhimu kuwa maandalizi ya mapema, matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa na ushirikiano wa sekta mbalimbali ni nguzo muhimu katika kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na matukio makubwa ya hali ya hewa.
MKULIMA WA RUKWA ANAVYTOTUIA UTABIRI
Mkulima katika Mkoa wa Rukwa Anansgisye Kalindile (66), ambaye ni mstafuu anasema kuwa anatumia taarifa za utabiri wa hali ya hewa TMA kama nyenzo muhimu katika kupanga shughuli zake za kilimo, kuanzia maandalizi ya shamba, uchaguzi wa mbegu, muda wa kupanda hadi kuvuna mazao.
Anasema kuwa kwa kuwa Rukwa ni miongoni mwa mikoa inayotegemea kwa kiasi kikubwa shughuli za kilimo, matumizi ya taarifa za hali ya hewa yanaweza kumsaidia mkulima kufanya maamuzi sahihi kuhusu wakati unaofaa kuanza kulima na kupanda mazao kama mahindi, maharage na alizeti.
“Ninapata mafanikio kutokana na kufuatilia tabiri zinazotolewa na TMA, kwani zimekuwa msaada mkubwa kwangu, hivi sasa tumepewa angalizo la uwepo wa mvua kubwa za El nino hivyo imenisaidia kujipanga katika kilimo na hata namna ya kujikinga nazo” anasema.
Elizabeth Mmbando (51) ni mkubwa wa mahindi eneo la Kibaingwa mkoani Dodoma, anasema kuwa kupitia utabiri wa msimu wa masika, ameweza kujua matarajio ya mvua katika eneo lake na kupanga muda wa kuandaa mashamba ili kuepuka kupanda mapema kabla ya mvua za kutosha kuanza au kuchelewa kupanda na hivyo kuathiri ukuaji wa mazao.
Anasema kuwa taarifa za utabiri wa siku 10 na kila mwezi zinamsaidia kufuatilia mabadiliko ya mwenendo wa mvua, kupanga matumizi ya mbolea, kufanya palizi na kuamua wakati mwafaka wa kutumia dawa za kudhibiti visumbufu vya mazao.
“Endapo utabiri unaonesha uwezekano wa mvua nyingi,huchukua tahadhari kwa kuweka mifereji ya kuondoa maji mashambani, kutumia matuta na kuchagua maeneo yasiyotuamisha maji ili kupunguza athari za mafuriko na kuoza kwa mizizi ya mimea.
Vilevile, taarifa zinazoonesha uwezekano wa mvua kupungua zinaweza kunisaidia kupanga matumizi ya maji, kuchagua mbegu zinazostahimili ukame na kuharakisha shughuli za shambani zinazohitaji unyevunyevu wa kutosha.
Anaongeza kuwa kwa upande wa uvunaji, utabiri wa hali ya hewa unaweza kumsaidia kupanga muda wa kuvuna, kukausha na kuhifadhi mazao ili kuepuka kuharibika kutokana na mvua zisizotarajiwa.
Hata hivyo, matumizi ya utabiri wa hali ya hewa yanahitaji mkulima kufuatilia taarifa rasmi za TMA na kupata ushauri kutoka kwa maafisa ugani ili kuzitafsiri kulingana na mazingira ya eneo lake.


