Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Novemba 1, 2026

TIMU ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid) katika Manispaa ya Kibaha, ikiongozwa na Wakili Revocatus Thadeo Mathew, imepokea na kushughulikia migogoro 94 katika kata tano, huku wananchi zaidi ya 2,500 wakipatiwa elimu ya msaada wa kisheria.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa kampeni hiyo ya awamu ya pili kwa siku nne za awali, Mathew alisema kati ya migogoro 94 iliyopokelewa, migogoro 45 imepatiwa ufumbuzi, huku 49 ikiendelea kushughulikiwa na timu ya watoa huduma za kisheria.

Alisema kampeni hiyo imefikia Kata za Mbwawa, Visiga, Misugusugu, Kongowe na Kibaha, ikilenga kutoa elimu ya sheria, ushauri na msaada wa kisheria kwa wananchi ili kuwasaidia kutambua haki zao na kupata ufumbuzi wa migogoro mbalimbali kwa njia sahihi za kisheria.

Aidha, alisema kampeni hiyo imefikia shule mbalimbali, zikiwemo Shule ya Sekondari Mbwawa, Shule ya Msingi Miswe Chini na Shule ya Sekondari Visiga, ambapo wanafunzi 3,188 na walimu 130 wamepatiwa elimu ya sheria ili kuwajengea uelewa wa haki zao na namna ya kuzilinda.

Katika hatua nyingine, timu hiyo Novemba 1, 2026, imefikia makanisa 10, ikiwemo Kanisa la Mtakatifu Dominic la Anglikana, ambako waumini walipatiwa elimu mbalimbali za kisheria wakati wa ibada ya Jumapili, huku wenye uhitaji wa kutatuliwa migogoro yao wakipatiwa huduma.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Diwani wa Kata ya Kibaha, Omary Bula, aliwapongeza watoa huduma kwa kufikisha huduma hizo katika kata yake, huku akitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuwezesha wananchi kupata huduma hizo.

Naye Mwanasheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, John Bundala, akitoa elimu kwa wajumbe wa mabaraza ya usuluhishi, alisema wajibu wa mabaraza hayo ni kusaidia wanandoa kufikia maridhiano katika kutatua migogoro yao.

Kampeni ya Samia Legal Aid awamu ya pili katika Manispaa ya Kibaha inaendelea kwa siku 10, kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 7, 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kisheria na kutatua migogoro yao kwa njia sahihi, bure na kwa wakati.