Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro

ASASI ya Kiraia ya SUHODE Foundation ya mkoani Morogoro imezitaka taasisi za fedha nchini kuweka na kutekeleza sera madhubuti zitakazohakikisha mikopo inayotolewa inazingatia uhifadhi wa mazingira, haki za binadamu na misingi ya maendeleo endelevu.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa SUHODE Foundation, Frank Luvanda, wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu uendelevu, uchumi wa buluu, uhifadhi na mazingira.

Luvanda amesema taasisi za fedha zinapaswa kuhakikisha wanaokopa wanaeleza namna watakavyotumia fedha wanazopatiwa ili kuepusha uwekezaji unaoweza kusababisha uharibifu wa mazingira.

“Sisi kama asasi za kiraia tumekuwa tukifanya kazi na mabenki na kukutana nao kwa nyakati mbalimbali kupitia WWF. Tunahamasisha mabenki yawe na sera madhubuti za kuhakikisha kila anayekopa anaeleza dhahiri kuwa hatatumia fedha hizo kuharibu mazingira. Hii ndiyo dhana ya ufadhili wa kijani (Green Financing),” amesema.

Amesema SUHODE Foundation imekuwa ikinufaika na ushirikiano wa muda mrefu na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (WWF), kupitia mafunzo, ziara za kujifunza kwa vitendo katika maeneo mbalimbali na wakati mwingine kupata msaada wa kifedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya uendelevu.

Amesema kwa sasa asasi hiyo imejikita katika masuala ya uendelevu na ESG, inayojumuisha mazingira, jamii na utawala bora, pamoja na usimamizi wa sheria zinazohusiana na uhifadhi.

Aidha, Luvanda ameishukuru Serikali kwa kuweka Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.

Amesema matumizi ya nishati chafu, ikiwemo kuni na mkaa, yana athari kwa mazingira na afya za watumiaji, hususan wanawake ambao kwa kiasi kikubwa wanahusika na shughuli za kupika.

“Tunapoharibu mazingira tunajiharibia sisi wenyewe. Kesho yetu na ya vizazi vijavyo inakuwa ngumu,” amesema.

Ameeleza kuwa matumizi ya muda mrefu ya kuni na mkaa yanaweza kusababisha magonjwa ya mfumo wa upumuaji kutokana na moshi unaozalishwa wakati wa kupika.

Amesema SUHODE Foundation imekuwa ikihamasisha matumizi sahihi ya nishati safi, akibainisha kuwa pamoja na kuwa na nishati bora, mazingira ya kupikia yanapaswa kuzingatiwa ili kuongeza ufanisi wa matumizi yake.

“Tumekuwa tukihamasisha matumizi bora na sahihi ya nishati. Unaweza kuwa na gesi asilia lakini ukiipikia mahali pa wazi ambapo upepo unapuliza, ufanisi wake unapungua,” amefafanua.

Kuhusu uhifadhi wa mazingira, Luvanda amesema SUHODE Foundation kwa kushirikiana na WWF na waandishi wa habari imekuwa ikihamasisha urejeshaji wa maeneo yaliyoharibiwa kwa kupanda miti ya matunda na biashara.

Ametaja maeneo ya kandokando ya mito na milima iliyoharibiwa kuwa miongoni mwa maeneo yanayohitaji kurejeshwa kupitia upandaji miti, ikiwemo miparachichi.

Akizungumzia uchumi wa kijani na buluu, Luvanda amesema WWF Tanzania imekuwa na mchango mkubwa katika kuhamasisha dhana hizo, ambazo zina manufaa kwa jamii na maendeleo ya taifa.

Amesema WWF imekuwa ikishirikiana na taasisi za fedha kuhakikisha huduma na bidhaa zao, ikiwemo mikopo, zinazingatia misingi ya uendelevu, uhifadhi wa mazingira na bioanuwai.

“Mikopo inapaswa kuwa na manufaa kwa mkopaji na benki ibaki na sura chanya,” amesema.

Kuhusu uchumi wa buluu, Luvanda amezipongeza Serikali ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuweka sera na miongozo inayolenga kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali za majini.

Ametolea mfano wa utaratibu wa kupumzisha maeneo ya uvuvi wa pweza, akisema hatua hiyo imesaidia kuongeza idadi ya pweza na kuboresha kipato cha wananchi wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi.

“Mfano mzuri ni upumzishaji wa miamba ya pweza. Serikali imekubali kutusaidia. Upumzishaji huo umesaidia kuongeza idadi ya pweza na kipato cha mwananchi. Hata Ziwa Victoria sasa linapumzishwa ili samaki wapate nafasi ya kukua na kuzaliana,” amesema.

Luvanda amehitimisha kwa kuishukuru WWF, asasi za kiraia, Serikali za Mitaa, halmashauri na majiji kwa ushirikiano wao katika kuhamasisha na kutekeleza ajenda ya uchumi wa buluu na uhifadhi wa mazingira.