Na Theophilida Felician, JamhuriMedia, Mara.

Wataalamu watiba asili na tiba mbadala
wametakiwa kuwa makini na kujiepusha mambo yanaweza kuhatarisha maisha ya wagonjwa.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wataalamu wa Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini (TAMESOT) na Mratibu wa Hamasa ya Mafunzo ya Sayansi Shirikishi nafasi ya ngazi ya Taifa, Lukasi Joseph Mlipu wakati akizungumza na mwandishi wa Jamhuri Digital leo Novemba 2, 2026 mkoani Mara.

Katibu huyi amehitimisha ziara ya hamasa ya mafunzo hayo mkoani humo ambapo amesema katika ziara yake amehamasisha mambo kadhaa ikiwemo watalaamu wa tiba asili kuzingatia mambo muhimu wanapokuwa katika utendaji kazi wa kuwatibu wagonjwa hususani kuepuka vitu vinavyoweza kuchochea madhara kwa wateja.

Amesema kama vile kujiepushe na madai ya tiba yasiyothibitishwa, ahadi za kuponya magonjwa yote na vitendo vingine vinavyoweza kusababisha changamoto kwa maisha ya mgonjwa

Amesema ili kufanikiwa hayo ni pamoja na kuzingatia suala la kuheshimu usalama wa mgonjwa, kujenga utamaduni wa kutoa huduma kwa uadilifu, kuelewa mipaka ya maarifa yao na kuwaelekeza wagonjwa kupata huduma za hospitali pale inapohitajika.

Hata hivyo amesisitiza kuwa TAMESOT imeendelea kuwahimiza wataalamu hao kushirikiana na Serikali na wadau wa afya kwani tiba asili inapaswa kuendelezwa kwa ushirikiano, mawasiliano mazuri, utafiti na uzingatiaji wa sheria na taratibu zinazotumika nchini.

Ameongeza kuwa amewahimiza kujisajili na kushiriki mafunzo hayo yatakayofanyika Novemba 9 hadi 13, 2026 Musoma maana kila mtaalamu ana nafasi ya kuchangia mafanikio ya programu hii kwa kueneza taarifa sahihi na kuwahamasisha wenzake kuchukua hatua kwa ufanisi zaidi.

Amehitimisha kwa kauli ya “Tukumbuke tiba asili si uchawi, tiba asili si utapeli, maarifa ya jadi yanahitaji elimu, utafiti, uadilifu na matumizi salama
tukiungana, tukijifunza na kushirikiana, tunaweza kuchangia katika kuhifadhi maarifa yetu ya jadi na kuendeleza matumizi yenye uwajibikaji ya dawa za asili kwa manufaa ya jamii”amesisitiza Katibu Mkuu Mlipu.