Na Dennis Luambano, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, amezitaka nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu kuwapa wanawake nafasi yenye ushawishi katika uamuzi, mazungumzo ya amani na utatuzi wa migogoro huku akisisitiza maazimio yaambatane na hatua zinazotekelezeka na kupimika.
Kauli hiyo ameitoa alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, kufungua Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Wabunge Wanawake wa Ukanda wa Maziwa Makuu unaofanyika kuanzia leo Novemba 2–5, 2026, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa ca Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam.
Amesema wanawake ni viongozi, wapatanishi na wajenzi wa amani, hivyo ni muhimu kuondoa mila kandamizi, ubaguzi na vikwazo vya kiuchumi vinavyopunguza ushiriki wao.
Amesisitiza kuwa Tanzania inaendelea kuwawezesha wanawake kupitia fursa za uongozi, elimu, masoko, mitaji na mikopo yenye masharti nafuu.
Kwa upande wake, Rais wa Jukwaa la Mabunge la Ukanda huo na Spika wa Bunge la Angola, Adão de Almeida, amesisitiza ushiriki kamili wa wanawake katika kujenga amani ya kudumu.
Naye Mwenyeji wa mkutano, Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu, ametaka mahitaji ya wanawake na wasichana yazingatiwe katika sheria, sera na bajeti.
Mkutano huo unahudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwamo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Judith Tuluka, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) katika Ukanda wa Maziwa Makuu, Huang Xia, Rais wa kwanza wa Bunge la Umoja wa Afrika na Katibu Mkuu wa Mkutano wa Beijing wa Mwaka 1995, Balozi Dk. Gertrude Mongella na Spika mstaafu, Anne Makinda.
Pia unawakutanisha maspika, wabunge, mawaziri, mabalozi, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, washirika wa maendeleo na asasi za kiraia.
Kauli mbiu ya mkutano ni “Ukanda wa Maziwa Makuu Wenye Amani na Maendeleo.”












