Na Hamid Yassin, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mgogoro wa uchaguzi ndani ya Klabu ya Simba umeibua maswali kuhusu uhalali wa mchakato wa kupata viongozi, mamlaka ya wanachama, nafasi ya mwekezaji na utekelezaji wa katiba mpya ya klabu.
Mvutano kati ya uongozi wa Simba na Kamati ya Uchaguzi umeweka wazi tofauti za mitazamo kuhusu uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Januari 3, 2027.
Kwa klabu yenye historia kubwa, mamilioni ya mashabiki, wanachama, wadhamini na uwekezaji mkubwa, mgogoro huu unahitaji ufumbuzi unaozingatia katiba na masilahi ya Simba.
Kinachopaswa kupewa uzito si nani atashinda mvutano, bali namna ya kujenga mfumo wa uongozi wenye uwazi, uwajibikaji na mgawanyo wa mamlaka unaoeleweka.
Kiini cha mgogoro ni tofauti za tafsiri ya katiba na uhalali wa mchakato wa uchaguzi.
Katiba iliyofanyiwa marekebisho Novemba 30, 2025, na kuidhinishwa Februari 2026, imeleta mabadiliko katika nafasi ya wanachama, Baraza la Wadhamini na wawekezaji.
Miongoni mwa mabadiliko yaliyotajwa ni kuimarishwa kwa mamlaka ya Baraza la Wadhamini katika kusimamia mali za klabu kwa niaba ya wanachama na kuwekwa kwa mfumo unaohusisha wawekezaji wasiopungua watatu badala ya mmoja.
Hata hivyo, utekelezaji wa mabadiliko hayo umeibua tofauti kuhusu mamlaka ya vyombo mbalimbali na utaratibu wa kuhamia mfumo mpya.
Oktoba 28, 2026, Kamati ya Uchaguzi ya Simba ilitangaza ratiba ya uchaguzi mkuu wa Januari 3, 2027, ikieleza kuwa imezingatia matakwa ya katiba kuhusu uchaguzi wa viongozi kila baada ya miaka minne.
Lakini Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, alipinga mchakato huo, akidai kuwa ni batili na haramu.
Mangungu alieleza kuwa uongozi unaendelea na mashauriano na serikali kuhusu utekelezaji wa mabadiliko ya mfumo wa uongozi na uwekezaji kabla ya uchaguzi.
Tofauti hizo zinahitaji kutatuliwa kwa kuzingatia katiba na kanuni za klabu badala ya masilahi ya watu binafsi.
KWA HABARI ZAIDI ZA KINA SOMA JAMHURI LA NOVEMBA 3-9, 2026


