Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Programu ya Mageuzi ya Kimkakati ya Mazingira Endelevu Tanzania Kulekea Dira 2050, inatarajiwa kuchochea fursa zaidi ya 25,000 za ajira wakiwemo watu wenye ulemavu ifikapo mwaka 2030.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa ameeleza hayo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Yumna Mmanga Omar bungeni jijini Dodoma leo Novemba 04, 2026.

Katika swali hilo Mhe. Yumna alitaka kujua ni hatua gani zimechukuliwa kwa Watu wenye Ulemavu kupata ajira na fursa za kiuchumi katika uhifadhi wa mazingira, usimamizi wa taka na uchumi wa kijani.

Akiendelea kujibu swali hiyo Mhe. Kwagilwa alisema Serikalikupitia Ofisi ya Makamu wa Raisimefanya mapitio ya kisera na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya hifadhi za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Alitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na Mradi wa Usimamizi Jumuishi wa Mifumo Ikolojia, Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) ambao umezalisha takribani ajira za moja kwa moja 18,336, wakiwemo na watu wenye ulemavu.

Mradi wa SLR unalenga kuzuia vitendo vya uharibifu wa mazingira vikiwemo ukataji miti, uchomaji mkaa na uharibifu wa vyanzo vya maji kwa kuleta shughuli mbadala za kipato kwa wananchi, unaotekelezwa katika halmashauri za wilaya saba na mikoa yake mitano kwenye mabano ambazo ni Iringa Vijijini (Iringa), Mbeya, Mbarali (Mbeya), Wanging’ombe (Njombe), Sumbawanga Vijijini (Rukwa), Tanganyika na Mpimbwe (Katavi) katika vijiji 54. 

Naibu Waziri Kwagilwa alisema kuwa Serikali itaendelea kufanya mapitio ya kisera na ya kisheria ili kuhakikisha kuwa kundi la watu wenye ulemavu linapata fursa stahiki katika utekelezaji wa miradi ya hifadhi ya mazingira inayoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Sanjari na hilo, aliongeza kuwa Ofisi hiyo pia inaendelea kutekeleza miradi ambayo ni jumuishi inayohusisha kundi la watu wenye ulemavu ambapo katika usimamizi na wake inatoa elimu ili watambue fursa zinazopatikana katika miradi hiyo.

Halikadhalika, alisema Serikali itaendelea kushirikiana na Uongozi wa kundi la Watu wenye Ulemavu ili waweze kuzifikia fursa hizi na waweze kushiriki moja kwa moja katika utekelezaji wa miradi.

Alisema hayo wakati akijibu swali la nyongeza alilouliza mbunge huyo akitaka kufahamu je, Serikali imechukua hatua gani kuhakikisha taasisi za watu wenye ulemavu zinatekeleza na kusimamia miradi ya mazngira nchini.

Kwa upande wake Mbunge Yumna alishauri pawe na mfumo wa utenganishaji wa takwimu ambao utanoesha kiasi gani watu wenye ulemavu wanavyonufaika na fursa za miradi ya mazingira nchini.