Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewapongeza wananchi wa mkoa huo kwa kudumisha amani na utulivu, akisema hali hiyo ni msingi muhimu wa kuendeleza shughuli za kiuchumi na kulinda nafasi ya Dar es Salaam katika kukuza uchumi wa Tanzania.

Amesema Dar es Salaam inachangia takribani asilimia 67 ya Pato la Taifa (GDP), hivyo amani na usalama katika mkoa huo vina umuhimu mkubwa si kwa wakazi wake pekee bali pia kwa uchumi wa taifa na nchi jirani zinazotegemea huduma zinazopatikana kupitia mkoa huo.

Akizungumza kuhusu umuhimu wa amani, Chalamila amesema Dar es Salaam ni kitovu cha shughuli nyingi za kiuchumi, ikiwemo biashara na huduma za bandari, ambazo zinazinufaisha nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Amezitaja nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Malawi na Zambia kuwa miongoni mwa nchi zinazotegemea huduma za bandari ya Dar es Salaam kwa upatikanaji wa bidhaa muhimu, zikiwemo mafuta na dawa.

Amesema kuvurugika kwa amani katika mkoa huo kunaweza kuathiri upatikanaji wa huduma hizo, kuvuruga biashara na kusababisha madhara ya kiuchumi kwa Tanzania na mataifa mengine.

Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi kuendelea kulinda amani, kufanya shughuli zao za biashara bila hofu na kutoruhusu vitendo vinavyoweza kuvuruga utulivu wa mkoa huo.

Aidha, amewahimiza wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao, kulipa kodi na kuchangia maendeleo ya mkoa, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kutoa taarifa za vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama.

Katika hatua nyingine, Chalamila ameeleza kusikitishwa na tukio la kijana mmoja aliyekuwa akijishughulisha na biashara ya mikopo na uwekezaji kuuawa baada ya kushambuliwa na watu waliokuwa na silaha na kumpora mali zake.

Amesema kijana huyo alikuwa miongoni mwa wananchi walioamua kujiajiri kupitia shughuli za biashara, hivyo tukio hilo ni la kusikitisha na linapaswa kuwa fundisho kwa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda maisha na usalama wa watu wanaojitafutia kipato.

Ametaka wananchi na viongozi kushirikiana katika kutoa taarifa za uhalifu na kuhakikisha wahusika wa vitendo hivyo wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Amesisitiza kuwa Dar es Salaam inapaswa kuendelea kuwa mfano wa amani, utulivu na mazingira salama ya uwekezaji na biashara ili kulinda maendeleo yaliyofikiwa.