Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Elimu kwa Umma kuhusu Muungano ili kuwa na jamii yenye umoja, mshikamano na uzalendo sanjari na kuuimarisha Muungano.
Elimu inayotolewa inahusu hoja zilizopatiwa ufumbuzi ambapo hadi kufikia mwaka 2025/26 jumla ya hoja 24 kati ya hoja 25 zimepatiwa ufumbuzi na hoja moja iliyobaki inayohusu masuala ya fedha inaendelea kufanyiwa kazi.
Kauli hiyo imetolewa bungeni jijini Dodoma leo Novemba 06, 2026 na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa wakati akijibu swali la Mbunge wa Tumbatu Mhe. Juma Othmani Hija aliyeuliza Serikali ina mpango gani wa kuwaelimisha Wananchi Hoja zote zilizo kwisha kupatiwa ufumbuzi ili wazielewe.
Akijibu swali hilo Mhe. Kwagilwa alisema kuwa Serikali imechukua jitihada mahususi za kutoa elimu kwa umma kuhusu Muungano ikiwemo kueleza wananchi hoja zilizopatiwa ufumbuzi.
Alibainisha kuwa elimu ya Muungano imekuwa ikitolewa kupitia redio, televisheni, makala za magazeti, machapisho vikiwemo vitabu kuhusu Muungano, maonesho ya kitaifa, makongamano, vyombo vya usafiri ambavyo ni treni ya kisasa ya SGR, boti za Azam Marines na mitandao ya kijamii.
Halikadhalika, Naibu Waziri Kwagilwa alisema Ofisi ya Makamu wa Rais ina mpango wa elimu kwa umma inayotolewa katika maeneo mbalimbali ya nchi na kuyafikia makundi yote ya kijamii.
“Mheshimiwa Spika hivi sasa Ofisi yetu inao mpango kabambe wa kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya Muungano mkoa kwa mkoa wilaya kwa wilaya kwa kutumia njia mbalimbali na tutahakikisha wananchi wanapata elimu hii,” alisema Mhe. Kwagilwa.
Aliongeza kuwa kutokana na uwepo wa watengeneza maudhui wenye ushawishi kwa jamii hususan makundi ya vijana, Ofisi imeandaa maudhui ambapo hivi karibuni wananchi wataanza kuyapata kupitia kwa wadau hao.
Mhe. Kwagilwa alieleza hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mhe. Hija ambaye pamoja na kuipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mpango huo wa elimu, alitaka kujua kama kuna njia zingine za kutumia kufikisha elimu hiyo.



