Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Nov 5,2026

WATU watatu wamefariki dunia na wengine wawili hawajapatikana baada ya boti iliyokuwa imebeba watu 23 kuzama katika Mto Rufiji, mkoani Pwani, huku watu 18 wakiokolewa.

Miongoni mwa waliofariki ni mwanamke mwenye umri wa miaka 60, mwanafunzi wa Kidato cha Pili katika Shule ya Sekondari Mwaseni na mtoto wa miaka saba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Protas Mutayoba, amesema ajali hiyo ilitokea Novemba 4, 2026, saa 12 jioni katika eneo la Kijiji cha Mloka, Kata ya Mwaseni.

Anasema boti hiyo mali ya Kijiji cha Mloka ilikuwa ikiendeshwa na Nassoro Abdallah Mkandu (32), mkazi wa Mloka, ikiwa na watu 23 waliokuwa wakitoka mashambani kuelekea kijijini kupitia Mto Rufiji.

Mutayoba amewataja waliofariki kuwa ni Sikitiko Naimbu, Shushani Ibrahim Kitimai na Masha Ali Buriani, wote wakazi wa Mloka.

Amesema kati ya watu 18 waliookolewa, watatu ni wanaume na 15 wanawake, ambao wanaendelea na matibabu katika Zahanati ya Mloka. Waliopotea ni Faimu Ibrahim Kitimai (6) na Nusra Makuka (28).

Akieleza chanzo cha ajali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji,Luteni Kanal Fredrick Komba, ameeleza boti hiyo iligonga gogo lililokuwa ndani ya maji na kusababisha kupinduka na kuzama.

“Jeshi la Polisi Rufiji kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na wananchi linaendelea na juhudi za kuwatafuta watu wawili ambao hawajapatikana”.

Komba amesema miili ya waliofariki tayari imezikwa na kwamba taarifa zaidi kuhusu tukio hilo zitatolewa.

Vyombo vya usafiri majini vimetakiwa kuzingatia kanuni za usalama, ikiwemo kutobeba abiria kupita uwezo wa chombo na kuhakikisha wanatumia vifaa vya kujiokolea, hususan maboya.