Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari amesema kuwa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ina nafasi muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hivyo mpango Mkakati wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni lazima ukawe ni msaada mkubwa wa kuyafikia malengo tarajiwa ya Dira 2050.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyasema hayo wakati akifungua kikao kazi cha Menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kupitia Mpango Mkakati wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mwaka 2026/27-2030/31 kilichofanyika tarehe 5 Novemba, 2026 katika Ukumbi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Dodoma.

Mhe. Johari, amesema kuwa, ni muhimu Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakafahamu nafasi yao katika utekelezaji wa Dira 2050, kwa kuwa Sheria bora na wezeshi ni msingi na nyenzo muhimu ya kuyafikia malengo ya Dira 2050.

“Ninaelekeza Menejimenti kuandaa mpango wa namna Ofisi itakavyoshiriki katika kuwezesha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia majukumu yetu.” Alisema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameridhishwa na utendaji na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Menejimenti ya Ofisi ikiwemo kuimarisha ushiriki wa Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika mafunzo mbalimbali yenye lengo la kuwajengea uwezo na kuboresha utendaji kazi wa watumishi hao.

Awali, akimkaribisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Samwel M. Maneno, amesema kuwa Ofisi imejipanga kuimarisha utoaji wa huduma za kisheria za awali (Preventive Legal Services) kwa kuboresha miundo mbinu ya TEHAMA na kuzuia madhara ya kisheria kabla hayajatokea.

Mhe. Maneno ameeleza kuwa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itawekeza nguvu na kuyapa kipaumbele matumizi ya teknolojia ili kuiwezesha Ofisi kuendelea kuishauri Serikali vizuri katika masuala yote ya kisheria ndani ya nchi na sheria za kimataifa.

Vilevile, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesisitiza kuwa, Ofisi itaendelea kuwajengea uwezo Watumishi kwa kuwawezesha kushiriki katika mafunzo mbalimbali ya ndani na Kimataifa, ili kuimarisha na kuboresha utendaji kazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutoa huduma za kisheria zenye ubora na viwango vinavyoaminika.

“Katika kipindi cha miaka mitano ijayo tunataka kujenga uwezo na kujiamini kwa watumishi wa Ofisi yetu wanapokuwa wanatoa ushauri wa kisheria na tutajikita zaidi katika maeneo ya utafiti na kufanya mafunzo kwa kiwango kikubwa.” Amesema Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.