Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimetakiwa kuchukua tahadhari mapema ili kuepusha madhara yaliyotokea wakati wa mvua za El Niño za mwaka 2023/2024, zilizosababisha hasara iliyozidi dola za Marekani bilioni mbili na zaidi ya watu milioni 1.5 kuyahama makazi yao.
Wito huo umetolewa wakati wa ufunguzi wa Mkutano Maalumu wa Kisekta wa Kikanda kuhusu Kujiandaa na Kukabiliana na Athari za Mvua za El Niño, uliofanyika jijini Nairobi, Kenya Novemba 05, 2026.
Mkutano huo wa ngazi ya Makatibu Wakuu ulilenga kuweka mikakati ya pamoja ya kujiandaa na kukabiliana na athari za mvua hizo, kwa kuzingatia kuwa majanga ya aina hiyo hayaheshimu mipaka ya nchi na hivyo yanahitaji uratibu na ushirikiano wa kikanda.
Tanzania iliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Bw. Charles Kadonya.
Katika kukabiliana na athari zinazotarajiwa, nchi wanachama zimetakiwa kulinda miundombinu muhimu ya usafirishaji na nishati inayounganisha nchi za ukanda huo, kuimarisha akiba ya chakula, kuwawezesha wakulima pamoja na kuwekeza katika miundombinu ya kuvuna na kuhifadhi maji.
Vilevile, zimesisitizwa kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ili kuzuia milipuko ya magonjwa yanayoweza kuongezeka kutokana na mafuriko, yakiwemo kipindupindu na malaria.
Kwa upande wake, Tanzania iliwasilisha mpango kazi wake wa kukabiliana na athari za El Niño na kueleza utayari wa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mpango kazi wa kikanda ulioandaliwa kupitia mkutano huo.
Mpango huo unalenga kuratibu hatua za dharura na kutambua maeneo ya kipaumbele ili kuhakikisha rasilimali zinazohitajika zinapatikana kwa wakati na kuwezesha nchi wanachama kulinda maisha na mali za wananchi.







