Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mkoa wa Dar es Salaam umeweka mikakati ya kujenga masoko makubwa ya kimkakati katika maeneo mbalimbali, yakiwemo Tandika na Bagamoyo, kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na kuwapatia wafanyabiashara wadogo maeneo rasmi ya kufanyia shughuli zao.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Oktoba 6,2026 Jijini Dar es salaam Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam RC Albert Chalamila amese.a Mpango huo unatarajiwa kutekelezwa kwa kutumia fedha za Serikali pamoja na ushirikiano na sekta binafsi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza biashara, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa wananchi.

Akizungumza kuhusu mipango hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema Serikali imeweka utaratibu wa kuendeleza miundombinu ya biashara ili wafanyabiashara waweze kufanya shughuli zao katika mazingira bora na yanayotambulika kisheria.

Amesema miongoni mwa miradi itakayoanza ni ujenzi wa masoko makubwa katika maeneo ya Tandika na Bagamoyo, huku Bagamoyo pia kukitarajiwa kujengwa stendi ya mabasi yenye thamani ya Sh bilioni 16 ili kurahisisha usafiri na shughuli za kibiashara.

“Serikali imepanga kujenga soko kubwa litakalokuwa na uwezo wa kuhudumia wafanyabiashara wadogo zaidi ya 12,000, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya ukosefu wa maeneo rasmi ya biashara. na kuondokana kupanga bidhaa chini”amesema RC Chalamila

Katika hatua nyingine, amesema kuna mpango wa kujenga soko katika eneo Mbagala kutajengwa Stendi ya Mabasi na ujenzi wa Soko la Mbagala litakalokuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara wasiopungua 4,000, huku fedha za mradi huo zikiwa katika hatua za kuandaliwa kwa ajili ya matumizi yaliyokusudiwa.