Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani linawashikilia watu kadhaa kwa mahojiano kufuatia matukio matatu tofauti ya vifo, likiwemo la mtoto wa miaka mitano anayedaiwa kuuawa kwa kupigwa na mama yake wa kambo, mtoto kunyweshwa pombe ya kienyeji na mfanyakazi wa kituo cha mafuta aliyeuawa kwa kushambuliwa na watu wasiojulikana.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amesema katika tukio la kwanza, muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe, Irine Machumu (32), anashikiliwa kwa tuhuma za kusababisha kifo cha Blessing Albert Mkisi, mkazi wa Msumbiji, Kisarawe, baada ya kudaiwa kumpiga kwa fimbo Novemba 2, mwaka huu, akimtuhumu kuchezea maji yaliyokuwa kwenye beseni pamoja na pacha wake.
Katika tukio jingine, Polisi wanawashikilia watu watatu, Bahati Shabani (32), Rehema Gabriel (37) na Elizabeth Dibison (35), wakazi wa Kijiji cha Kwaruhombo, Chalinze, kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha Mustapha Mubaraka (3), aliyedaiwa kunyweshwa pombe ya kienyeji aina ya wanzuki Oktoba 30, mwaka huu, akiwa pamoja na watoto wengine wawili nyumbani kwa mama yake mkubwa.
Kamanda Morcase amesema baada ya kunywa pombe hiyo, Mustapha alizidiwa na kukimbizwa katika zahanati ya kijiji kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Msoga, ambako alifariki dunia Oktoba 31, huku Polisi wakichunguza mazingira ya tukio na uhusiano wa kifo hicho na pombe aliyodaiwa kunyweshwa.
Aidha, katika tukio la tatu, mfanyakazi wa kituo cha mafuta cha ORYX, Jimmy Lema (29), amefariki dunia baada ya kushambuliwa kwa kitu chenye ncha kali na watu wasiojulikana akiwa kazini eneo la Kibosha, Mapinga, Wilaya ya Bagamoyo, Novemba 5, 2026, majira ya saa 3:15 usiku.
Amesema marehemu alikuwa zamu ya usiku pamoja na mfanyakazi mwenzake aliyetajwa kwa jina la Junior John, ambapo baada ya kupungua kwa wateja alikwenda kupumzika ndani ya kituo hicho, lakini baadaye alivamiwa na kushambuliwa hadi kupoteza maisha.
Jeshi la Polisi linaendelea na msako wa kuwatafuta waliohusika na tukio hilo ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.



