Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
Novemba 8,2026

MWAJUMA Rashid (67), mkazi wa Maili Moja, Manispaa ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid), iliyomuwezesha kupata msaada baada ya kudai kufanyiwa vitendo vya ukatili na binti yake wa kumzaa.

Mwajuma anasema awali alimpatia binti yake, Siwazuri Khatibu (43), kiwanja kwa nia ya kumsaidia kuwa na makazi, lakini baadaye uhusiano wao uligeuka kuwa mgogoro, akidai kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo kupigwa na kukabwa koo. Juhudi zake za kutafuta suluhu katika maeneo mbalimbali hazikuzaa matokeo aliyoyatarajia.

Hata hivyo, baada ya kufika katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria lililokuwa kwenye kampeni hiyo Maili Moja, alisikilizwa na kupatiwa msaada pamoja na maelekezo ya kisheria, hatua iliyofuatwa na binti yake kuchukuliwa na vyombo vya dola siku iliyofuata.

Akizungumza Novemba 7, 2026, wakati wa kuhitimisha kampeni hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani (RAS), Richard Kayombo, alisema jumla ya wananchi 380,874 wamefikiwa na huduma za msaada wa kisheria katika wilaya saba na halmashauri tisa za mkoa huo ndani ya siku 10 za utekelezaji wa awamu ya pili ya kampeni hiyo.

Alisema kati ya waliofikiwa, wanawake ni 196,410 na wanaume 184,464, huku wananchi wakipata fursa ya kuwasilisha kero, kupata ushauri wa kisheria na baadhi ya migogoro kutatuliwa papo kwa papo.

Kayombo alibainisha kuwa jumla ya migogoro 426 ilipokelewa, ikihusu mashauri ya madai na jinai, usimamizi wa mazingira, utawala bora, ajira na kazi, mirathi pamoja na masuala ya ndoa.

Alisema idadi hiyo imeongezeka ikilinganishwa na awamu ya kwanza iliyofikia wananchi 200,243, wakiwemo wanawake 101,967 na wanaume 98,276.

Kayombo aliahidi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuendelea kuwa karibu na wananchi katika kusikiliza na kushughulikia kero zao hata baada ya kukamilika kwa kampeni hiyo Novemba 7.