📍 NIRC: Arusha
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imeendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia na miundombinu ya Umwagiliaji kama njia muhimu ya kuongeza uzalishaji, ubora wa mazao na ushindani wa bidhaa za kilimo katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Ujumbe huo umetolewa kupitia ushiriki wa Tume katika Maonesho ya Kimataifa ya Horti Logistica Africa yanayofanyika katika Viwanja vya TGT, Burka jijini Arusha, yaliyozinduliwa leo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi.
Kupitia maonesho hayo, NIRC imeeleza kuwa uwepo wa miundombinu imara ya Umwagiliaji ni muhimu katika kuwawezesha wakulima wa matunda, mbogamboga na maua kuzalisha kwa uhakika mwaka mzima, kuongeza mavuno na kukidhi mahitaji ya masoko yenye ushindani.
Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja Umwagiliaji Mkoa wa Arusha, William Kidinda, amesema Umwagiliaji ni nguzo muhimu katika kufanikisha mapinduzi ya kilimo nchini kwa kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji na kufanya kilimo kuwa shughuli endelevu ya kibiashara.
“Umwagiliaji unawawezesha wakulima wa matunda, mbogamboga na maua kuendelea kuzalisha hata wakati wa ukame au mvua zisizotabirika. Hali hii husaidia kuongeza kiasi na ubora wa mazao, hivyo kuwaongezea wakulima fursa ya kupata masoko na kuongeza kipato,” amesema Kidinda.
Aidha, wataalamu wa NIRC wameeleza kuwa matumizi ya teknolojia za Umwagiliaji ni sehemu ya mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuongeza kipato cha wakulima na kuimarisha usalama wa chakula na lishe nchini.
Maonesho hayo yamewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya hortikultura kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujadili fursa za biashara, teknolojia na uwekezaji katika sekta hiyo. Kupitia ushiriki wake, NIRC inaendelea kutoa elimu kuhusu matumizi endelevu ya maji pamoja na fursa za uwekezaji katika miundombinu ya Umwagiliaji kwa maendeleo ya wakulima na uchumi wa Taifa.











