Na Kulwa Karedia, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Matumizi mabaya ya fedha za umma katika halmashauri nchini yameendelea kuwa changamoto kubwa, huku mabilioni ya fedha yakipotea.

Kadhalika, mapato yamekuwa yakikusanywa chini ya malengo na baadhi ya watumishi na mawakala wa ukusanyaji wakitajwa kushindwa kutekeleza wajibu wao.

Mbali na upotevu huo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeibua dosari katika usimamizi wa fedha za halmashauri, ikiwamo ucheleweshaji wa uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha, kutorejeshwa kwa sehemu ya kodi ya ardhi na matumizi yanayozidi bajeti katika klabu za soka zinazomilikiwa na halmashauri.

Katika taarifa yake ya ukaguzi wa fedha kwa mwaka 2023/2024 na 2024/2025 iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma wiki iliyopita, kamati hiyo imetaka hatua madhubuti zichukuliwe ili kuziba mianya ya upotevu wa fedha za umma na kuwawajibisha wote watakaobainika kuhusika.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Mwenyekiti wa LAAC, Addo Shaibu, amesema bado kuna upotevu mkubwa wa fedha za umma katika halmashauri, huku hatua zinazochukuliwa dhidi ya wahusika zikiwa haziridhishi.

“Bado kuna upotevu mkubwa wa fedha za umma katika halmashauri zetu, hakuna hatua stahiki zinazochukuliwa dhidi ya wahusika,” amesema.

Amesema licha ya Serikali Kuu kutoa fedha kwa ajili ya kuziwezesha halmashauri kutekeleza shughuli za maendeleo, ukusanyaji wa mapato ya ndani haukuwa wa kuridhisha.

Kwa mujibu wa Shaibu, uchambuzi wa kamati umebaini halmashauri nyingi hazifikii malengo ya ukusanyaji wa mapato kutokana na kukosekana kwa ubunifu wa vyanzo vipya endelevu, kushindwa kukusanya kikamilifu mapato katika vyanzo vilivyopo na kutodhibiti mianya ya upotevu wa fedha.

KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA JAMHURI LA NOVEMBA 10 – 16, 2026