Na Joel Mjengi, JamhuriMedia, Dodoma

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Daud Kalata, amesema maziwa si tiba ya vidonda vya tumbo, bali yanaweza kumpa mgonjwa ahueni ya muda mfupi bila kuondoa chanzo cha ugonjwa.

Amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakitumia maziwa kama tiba, huku wengine wakipuuzia dalili za ugonjwa huo na kuchelewa kupata matibabu hospitalini.

Akizungumza na JAMHURI mwishoni mwa wiki jijini Dodoma, Dk. Kalata amesema vidonda vya tumbo vinaweza kusababisha madhara makubwa endapo mgonjwa hatapata matibabu sahihi kwa wakati.

“Maziwa siyo tiba ya vidonda vya tumbo, bali huleta ahueni tu kwa mgonjwa. Hayana uwezo wa kuua kimelea ambacho hutibiwa kwa dawa maalumu,” amesema.

Ameeleza kuwa vidonda vya tumbo hutokea kwenye ukuta wa tumbo au sehemu ya kwanza ya utumbo mdogo, baada ya utando unaolinda maeneo hayo dhidi ya tindikali kuathirika.

Amesema miongoni mwa visababishi vikuu ni maambukizi ya bakteria aina ya Helicobacter pylori (H. pylori) na matumizi ya baadhi ya dawa za kupunguza maumivu bila ushauri wa daktari.

Ametaja dawa hizo kuwa ni pamoja na aspirin na ibuprofen, ambazo matumizi yake yasiyo sahihi yanaweza kuongeza hatari ya kupata vidonda vya tumbo.

Dk. Kalata amesema uvutaji sigara na unywaji pombe kupita kiasi vinaweza kuongeza matatizo kwa wagonjwa, huku akisisitiza umuhimu wa kufuata ushauri wa kitaalamu.

Amewataka wananchi kuzingatia usafi wa chakula na maji, ikiwamo kuosha mboga na matunda kwa maji salama ili kupunguza hatari ya maambukizi mbalimbali.