Na Hamid Yassin, JamhuriMedia, Arusha
Wiki iliyopita Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jijini Dodoma, lilishuhudia majibizano kuhusu gharama za ujenzi wa Uwanja wa Dk. Samia Suluhu Hassan, Arusha, unaotarajiwa kutumika katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.
Malumbano kati ya viongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na wabunge Mwita Waitara na Revocatus Chipando, maarufu Baba Levo, yameibua maswali yanayohitaji majibu ya kitaalamu, badala ya mashambulizi binafsi.
Swali la msingi ni hili: Je, mjadala kuhusu gharama za uwanja huo unasaidia kulinda fedha za umma na kuharakisha ujenzi, au unageuka kuwa mvutano unaofunika malengo ya mradi?
Hoja za wabunge hao kuhusu ongezeko la gharama zinastahili majibu ya kina kutoka serikalini, hasa kwa kuzingatia masuala yaliyowahi kuibuliwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kwa mujibu wa taarifa za ukaguzi, makadirio ya awali ya mradi yalikuwa Sh bilioni 187, lakini mkataba ulisainiwa kwa Sh bilioni 338.54, tofauti ya Sh bilioni 151.54.
Tofauti hiyo ni kubwa na inahitaji ufafanuzi unaoonyesha namna gharama zilivyokokotolewa, sababu za mabadiliko na taratibu zilizofuatwa kuidhinisha matumizi hayo.
Wabunge wanapohoji matumizi ya fedha za umma, wanatekeleza wajibu wao wa kuisimamia serikali. Vivyo hivyo, serikali ina wajibu wa kutoa majibu yanayoambatana na ushahidi.
Waziri Paul Makonda ameeleza kuwa ongezeko la gharama limetokana na mabadiliko ya mahitaji ya mradi na viwango vya kimataifa vinavyotakiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Ameeleza pia kuwa Sh bilioni 52 zinahusiana na kodi.
Hata hivyo, maelezo hayo yanapaswa kuungwa mkono na nyaraka zinazoonyesha gharama za kila kipengele kilichoongezwa au kubadilishwa. Hiyo ndiyo njia ya kuondoa shaka na kuweka mjadala katika msingi wa ukweli.
KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA JAMHURI LA NOVEMBA 10 – 16, 2026


