Dar es Salaam

Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) umepokea ujumbe kutoka Wizara ya Nishati ya Malawi uliotembelea Wakala huo Novemba 13, 2026, kwa lengo la kujifunza uzoefu wa Tanzania katika matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Ufuatiliaji na Udhibiti wa Shughuli za Upakuaji wa Mafuta (SCADA).

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Petroli wa PBPA, Mhandisi Bruno Tarimo, ameeleza namna mfumo huo unavyotumika kufuatilia na kudhibiti mchakato wa upakuaji wa mafuta kutoka kwenye meli kwenda kwenye matanki ya kuhifadhia mafuta katika bandari za Tanzania.

Amebainisha kuwa matumizi ya mfumo wa SCADA yameimarisha usimamizi wa shughuli za upakuaji wa mafuta kwa kuwezesha upatikanaji wa taarifa kwa wakati halisi, kuongeza usahihi wa vipimo na kupunguza uwezekano wa upotevu wa mafuta wakati wa mchakato huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Nishati kutoka Wizara ya Nishati ya Malawi, Joseph Kalowekamo, ameipongeza PBPA kwa kuwekeza katika matumizi ya teknolojia hiyo, akieleza kuwa ni hatua muhimu katika kuimarisha ufanisi, uwazi na usimamizi wa shughuli za upakuaji wa mafuta.

Amesema uzoefu walioupata kupitia ziara hiyo utakuwa chachu ya kujifunza na kubaini maeneo ambayo yanaweza kuboreshwa katika usimamizi wa shughuli za mafuta nchini Malawi.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kubadilishana uzoefu na maarifa kati ya Tanzania na Malawi katika sekta ya nishati, hususan matumizi ya teknolojia za kisasa katika kuimarisha usimamizi na ufanisi wa shughuli za mafuta.