Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Karatu
Zipo nyakati jamii hufika njia panda. Zipo nyakati taifa hufika njia panda. Zipo nyakati taifa huhitaji hekima kuliko misimamo au mifumo ya kisheria. Zipo nyakati taifa huhitaji busara zaidi kuliko kiburi au ushindi. Maandiko matakatifu yanasema zipo nyakati za kupanda, kupalilia na kuvuna.
Sitanii, Tanzania yetu imefika hapo tulipo. Leo ninawaambia CCM na CHADEMA, mkiamua, tunatoka. Viongozi wetu wakuu wanisamehe kwa kusema hili. Tunayoyaona leo yametokana na kudharau mwiba, sasa mguu umeota tende. Hatima ya nchi yetu iko mikononi mwenu.
Nianze na CHADEMA. Historia ni mwalimu mzuri, lakini humwadhibu mwanafunzi asiyependa kujifunza. NCCR-Mageuzi iliwahi kutikisa nchi. TLP ilipata kuwa gumzo. CUF iliwahi kujenga ushawishi mkubwa. Leo vyama hivi viko wapi kisiasa? Vilishindwa kusoma alama za nyakati na kutumia fursa kujijenga kuwa vyama vikuu vyenye uwezo wa kupokezana madaraka na CCM.
Angalieni Marekani. Republican na Democrat wamejenga mifumo inayowawezesha kupokezana madaraka. Uingereza, Labour na Conservative wamekuwa mihimili mikuu ya ushindani wa kisiasa. CHADEMA ina nafasi ya kujenga historia kama hiyo Tanzania.
Sitanii, kuna ukweli mchungu. Roma haikujengwa siku moja. Demokrasia nayo haijengwi kwa hasira za siku moja. Inahitaji subira, mazungumzo, kujitoa na wakati mwingine kukubali kupiga hatua moja nyuma ili kupiga hatua mbili mbele!
CHADEMA, msiiache fursa hii ipite. Leo ushawishi wenu umefikia kiwango kikubwa. Mna wafuasi, mna sauti na mna nafasi ya kuandika historia. Msirudie makosa ya waliowatangulia. Mlango wa maridhiano alioufungua Rais Samia Suluhu Hassan ndiyo njia sahihi. Ingieni, zungumzeni, dai haki zenu na mjenge mazingira ya ushindani wa kisiasa wenye tija.
Kusema hivyo, haimaanishi kuwa CCM hamna chembe ya lawama. Sote tulimsikia Jaji Mohamed Chande. Alieleza gunia la hasira lilipotokea katika taifa letu. Watu kuambiwa hawajui kusoma na kuandika ni tusi lisilosameheka, hata kama lilifanywa na awamu iliyotangulia. Ikumbukwe, CCM mna wajibu mkubwa zaidi. Ninyi mmeshika dola. Mnayo dhamana ya kulinda maisha, haki na umoja wa Watanzania wote, wakiwamo wanaowapinga.
Yaliyotokea Oktoba 29, 2025, yananing’inia migongoni mwenu. Vifo vya Watanzania katika mazingira ya kisiasa ni doa ambalo haliwezi kufutwa kwa hotuba, ukimya au kupita kwa muda. Linahitaji ukweli, haki, uwajibikaji na maridhiano ya dhati.
CCM haiwezi kujenga utawala wenye amani ya kudumu ikiwa majeraha hayo yataachwa bila kutibiwa. Vivyo hivyo, CHADEMA haiwezi kujenga ushindi wenye maana ikiwa gharama yake ni maisha ya Watanzania.
Sitanii, damu ya Mtanzania haina rangi ya chama. Anayekufa si kura ya CCM wala CHADEMA. Ni baba, mama, mtoto au ndugu wa mtu. Tanzania haikupaswa kufikia hapa.
Sitanii, kwa unyenyekevu mkubwa namwomba Rais Samia atumie mamlaka yake yaliyopo ndani ya Katiba na sheria kutafuta suluhu itakayomrejeshea Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, uhuru, hata kabla taratibu za rufaa hazijakamilika. Hatua hiyo inaweza kuwa daraja la kihistoria la maridhiano.
CHADEMA nao wasishupaze shingo. Maridhiano si kusalimu amri; ni ushindi wa busara. CCM nao wasione kulegeza msimamo kuwa udhaifu. Nguvu ya kiongozi hupimwa pia kwa uwezo wa kusamehe na kuunganisha watu.
Wote wakubali kubadilika inapobidi. Hakuna mshindi katika taifa linalolia.
Kwa sauti ya Makamu wa Rais Deogratias Ndejembi, wana Sitanii, Tanzania ni kubwa kuliko CCM na CHADEMA. Wanasiasa watapita, lakini taifa litabaki. CCM, CHADEMA, mkiamua tunatoka. Msipoamua, historia itawahukumu. Mungu ibariki Tanzania.
0784 404827

