📌 Shirika lafikisha wateja milioni 6 na uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 4,600.

📌• Lengo ni kuzalisha megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 na kumfikia kila Mtanzania.

📌Bodi ya TANESCO yaishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa na mageuzi ya sekta ya nishati.

Na, Mwandishi wetu

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Plasduce Mbossa, amesema maadhimisho ya miaka 95 ya TANESCO tangu kuanzishwa kwake yamekuwa ya mafanikio makubwa na ya kihistoria, hususan baada ya uzinduzi wa mradi mkubwa wa kimkakati wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) unaozalisha megawati 2,115.

Akizungumza kuhusu safari ya TANESCO iliyoanza rasmi Novemba 26, 1931, Bw. Mbossa amebainisha kuwa shirika la TANESCO limepiga hatua kubwa katika kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini.

“Leo Tanzania ina uwezo wa kuzalisha umeme zaidi ya megawati 4,600. Hii ndiyo maana halisi ya kaulimbiu yetu ya mwaka huu isemayo: Miaka 95 ya Kuliangazia Taifa,” amesema Bw. Mbossa.

Aidha, ameongeza kuwa wigo wa huduma wateja umepanuka kwa kasi ambapo kwa sasa TANESCO inahudumia wateja takribani milioni sita nchi nzima, sambamba na kufanya mageuzi makubwa ya kidijitali yaliyorahisisha na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Bw. Mbossa kwa niaba ya Bodi na Menejimenti ya TANESCO, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uwezeshaji wa kifedha, na maono thabiti katika kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.

Amesema mazingira wezeshi yaliyowekwa na Serikali ndiyo chachu iliyofanikisha kukamilika kwa miradi hiyo na kuleta mapinduzi ya nishati nchini.

Akizungumzia mwelekeo wa baadaye, Bw. Mbossa amesisitiza kuwa safari bado inaendelea, huku lengo kuu likiwa ni kuhakikisha taifa linafikisha uzalishaji wa megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030. Ameeleza kuwa hatua hiyo itakwenda sambamba na azma ya kumfikishia nishati ya umeme kila Mtanzania na kuwezesha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.