Serikali imekuwa mwanahisa mkubwa zaidi wa Kampuni ya Mikopo ya Nyumba Tanzania (TMRC) baada ya kukamilisha umiliki wa asilimia 27.73 ya hisa zake, takribani hisa 12,166,674 zenye thamani ya Sh17.76 bilioni.

Kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), Serikali sasa inaongoza orodha ya wanahisa 21 wa kampuni hiyo, yenye mtaji uliolipwa ‘a paid-up capital’ wa Sh56.02 bilioni.

Hati ya umiliki wa hisa ilikabidhiwa Alhamisi, Novemba 27, 2026, jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TMRC, Bw. Theobald Sabi, kwa Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu.

Akizungumza kabla ya kukabidhiwa hati hiyo, Bw. Mchechu alisema Serikali, kama mwanahisa wa kimkakati, inalenga kuiwezesha TMRC kupata fedha za muda mrefu na za gharama nafuu, kuongeza imani ya wawekezaji, na kuhakikisha inachangia Dira 2050, inayotaja makazi bora kuwa mojawapo ya malengo yake.

“Makazi ni chachu ya amani na ukuaji wa uchumi wa nchi. Tuna wajibu wa kuwainua Watanzania wengi ili kudumisha amani,” alisema, akisisitiza kuwa uwekezaji huo unathibitisha dhamira ya Serikali ya kutatua changamoto ya nyumba nchini.

Bw. Mchechu alisema imani ya wawekezaji kwa Tanzania inatokana na sera nzuri za kiuchumi, na akaitaka TMRC itumie fursa hiyo kujipambanua kwa kuendelea kutoa hati fungani.
Aliitaka pia kampuni hiyo kushirikiana na benki kubuni bidhaa mpya zitakazowawezesha wananchi wengi zaidi kumudu gharama za nyumba.

Kwa upande wake, Bw. Sabi alisema hatua ya Serikali kununua hisa za TMRC, ni uthibitisho wa imani ya Serikali kwa kampuni hiyo na itaiongezea uwezo wa kuzisaidia benki na taasisi za fedha kutoa mikopo ya nyumba ya muda mrefu na kwa gharama nafuu.

“Huu si uwekezaji kwenye nyumba pekee, bali katika mapambano dhidi ya umaskini, kwani sekta ya nyumba inabeba sekta nyingine nyingi,” alisema, akiahidi kuwa Bodi itaendelea kuisimamia taasisi hiyo kwa weledi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TMRC, Bw. Elibariki Ndossi, alisema hadi Septemba 30, 2026, kampuni hiyo ilikuwa imezikopesha benki na taasisi za fedha Sh209.47 bilioni, sawa na takribani asilimia 26 ya soko la mikopo ya nyumba nchini.

Sehemu kubwa ya fedha hizo, Sh128.2 bilioni, ilitokana na Mradi wa Kufadhili Mikopo ya Nyumba (HFP) wa Benki ya Dunia.

Mradi huo ulianza mwaka 2010 kwa mkopo wa masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 40 kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa (IDA), ukaongezewa fedha hadi takribani dola milioni 100, na kufungwa Juni 28, 2019.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), iliyokuwa taasisi tekelezi ya mradi huo, iliipa TMRC leseni mwaka 2011 na inaendelea kuisimamia chini ya Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya 2006 na Kanuni za Makampuni ya Kufadhili Mikopo ya Nyumba za 2022.
Bw. Ndossi alisema tangu wakati huo, mtaji wa TMRC umeongezeka kutoka Sh2.9 bilioni hadi Sh56.02 bilioni, huku idadi ya benki zinazotoa mikopo ya nyumba ikipanda kutoka tatu hadi 30.

Hata hivyo, alionya kuwa ukuaji wa mikopo ya nyumba hauendani na ongezeko la nyumba zenyewe.

“Fedha za mikopo peke yake hazijengi nyumba. Nyumba lazima zijengwe kwanza, kwa bei ambayo wananchi wanaweza kumudu, ndipo mikopo ya nyumba iwe na maana,” alisema.

Takwimu alizozitoa zinaonesha ukubwa wa pengo hilo. Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi ya Watu (UN-Habitat) linakadiria kuwa Tanzania ina upungufu wa takribani nyumba milioni nne, huku Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikisema nchi inahitaji nyumba mpya 391,000 kila mwaka.

Kwa mujibu wa Wizara hiyo, mwaka 2022 nchi ilikuwa na takribani nyumba milioni 14.7 kwa watu milioni 61.7.

Mahitaji hayo yanatarajiwa kuongezeka zaidi kwani ifikapo 2050, idadi ya watu itafikia milioni 118.1 na mahitaji ya nyumba milioni 26.8, huku asilimia 59 ya Watanzania wakitarajiwa kuishi mijini, kutoka asilimia 34.9 mwaka 2022.

Shinikizo hilo tayari linaonekana mijini. Sensa ya 2022 inaonesha kuwa asilimia 43.1 ya kaya za mijini zina chumba kimoja tu cha kulala, na ni asilimia 12.2 tu ya kaya zenye hati miliki.

Kwa upande wa fedha, soko la mikopo ya nyumba bado ni dogo. Deni la mikopo hiyo ni asilimia 0.45 tu ya Pato la Taifa, na wastani wa mkopo mmoja ni Sh138 milioni.

Ingawa riba zimeshuka kutoka asilimia 20–24 hadi 13–18, bado ni mzigo kwa kaya nyingi.

Hata hivyo, Ndossi alisema changamoto hiyo si ya Tanzania pekee. UN-Habitat inakadiria kuwa duniani kote watu bilioni 2.8 hawana makazi bora ya kutosha, na zaidi ya bilioni 1.1 wanaishi katika makazi duni.

Barani Afrika, asilimia 62 ya makazi ya mijini si rasmi, na Benki ya Shelter Afrique inakadiria upungufu wa bara hilo kuwa zaidi ya nyumba milioni 53. Ili kukidhi mahitaji ifikapo 2030, dunia ingehitaji kujenga takribani nyumba 96,000 kila siku.

Kukabili hali hiyo nchini, alisema Serikali imeendelea kujenga mazingira wezeshi, ikiwemo Sera ya Taifa ya Ardhi, kuondoa kodi kwenye ujenzi wa nyumba zenye thamani ya chini ya Sh50 milioni, na kuboresha utoaji wa hati za sehemu ya nyumba (unit titles).

Ofisi ya Msajili wa Hazina na TMRC zimesema zitaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha, BoT na taasisi za fedha kujenga mfumo imara na endelevu wa ufadhili wa makazi.

Akimwakilisha Gavana wa BoT, Naibu Gavana anayesimamia Uthabiti wa Sekta ya Fedha, Sauda Msemo, alisema benki hiyo inatarajia TMRC kuendeleza mafanikio yake katika kuboresha sekta ya makazi na mfumo wa fedha nchini.
“TMRC ni wakala muhimu katika kutekeleza Dira 2050 kwani ni mdau mkubwa katika ukuaji wa sekta ya makazi,” alisema.