Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeibuka miongoni mwa washindi wa tuzo za ubora wa uwasilishaji wa taarifa za fedha kwa mwaka 2025, katika kundi la Mashirika ya Umma ya Kibiashara yanayotumia Viwango vya Kimataifa vya Utoaji wa Taarifa za Fedha (IFRS).

Tuzo hizo, zilizoandaliwa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA), zimeitambua TANESCO kwa kuzingatia viwango na misingi ya kitaalamu katika uandaaji na uwasilishaji wa taarifa za fedha, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Shirika katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na utawala bora.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO – Usambazaji Umeme, Mhandisi Timothy Mgaya, amesema mafanikio hayo ni matokeo ya juhudi za pamoja za Shirika katika kuimarisha usimamizi wa rasilimali na kuzingatia viwango vya kitaalamu katika utendaji wake.

“Tuzo hii ni alama tosha inayothibitisha juhudi ambazo TANESCO imekuwa ikizifanya katika kuhakikisha tunazingatia misingi na viwango vilivyowekwa na bodi hii. Pia, inathibitisha uwepo wa utawala bora ndani ya Shirika, unaojengwa katika misingi ya uadilifu na uongozi thabiti,” amesema Mhandisi Mgaya.

Ameongeza kuwa Shirika litaendelea kudumisha ubora katika uandaaji na uwasilishaji wa taarifa za fedha, sambamba na kuimarisha mifumo ya usimamizi na uwajibikaji.

Mafanikio hayo yanaakisi dhamira ya TANESCO ya kuimarisha utendaji wa kitaasisi, kusimamia rasilimali kwa ufanisi na kujenga imani ya Serikali, wateja na wadau mbalimbali wa Shirika.