Na Mwandishi Wetu, DODOMA
TAASISI ya Watumishi Housing Investment (WHI) imetumia mbio za NHIF Marathon 2026 zilizofanyika jijini Dodoma kutangaza huduma zake, kutoa elimu kuhusu fursa za uwekezaji na kuhamasisha wananchi kujipatia makazi bora kupitia miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba inayotekelezwa nchini.
Ushiriki wa taasisi hiyo katika mbio hizo zilizofanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 25 ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umelenga kuisogeza karibu na wananchi kwa kuwapa fursa ya kufahamu shughuli zake, huduma zinazotolewa pamoja na namna wanavyoweza kunufaika na uwekezaji katika sekta ya nyumba.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, mwakilishi wa WHI, Stephen Mkande, amesema taasisi hiyo imeona umuhimu wa kutumia majukwaa kama NHIF Marathon kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuwajengea uelewa kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana kupitia taasisi hiyo.
Amesema WHI inajihusisha na maeneo mbalimbali ya uwekezaji, ikiwemo uwekezaji wa pamoja kupitia mfuko wa Faida Fund, unaowezesha Watanzania kushiriki katika uwekezaji na kupata fursa ya kukuza mitaji yao.
Aidha, amesema taasisi hiyo inatekeleza miradi ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kwa lengo la kuwawezesha watumishi wa umma na wawekezaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii kupata fursa ya kumiliki makazi bora.
Ameeleza kuwa miradi hiyo inatekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza na Morogoro, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupanua upatikanaji wa nyumba na kukuza uwekezaji katika sekta ya makazi.
Akizungumzia miradi inayotekelezwa jijini Dodoma, Mkande amesema baadhi ya nyumba zinaendelea kujengwa, huku nyingine zikiwa tayari zimewekwa sokoni ili kutoa fursa kwa wananchi na wawekezaji wenye nia ya kuzinunua.
Katika hatua nyingine, amewahimiza wananchi na washiriki wa NHIF Marathon 2026 kutembelea banda la WHI ili kupata ufafanuzi kuhusu miradi ya nyumba, huduma za taasisi hiyo na utaratibu wa kushiriki katika fursa za uwekezaji zinazotolewa.
Ushiriki wa WHI katika mbio hizo ni sehemu ya juhudi za taasisi hiyo kuimarisha uhusiano na jamii, kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu uwekezaji na kuhamasisha umiliki wa nyumba bora kupitia fursa zinazopatikana nchini.







