Mpita Njia (MN) amepata fursa ya kwenda
Uwanja wa Ndege wa zamani wa Dar es
Salaam (Terminal I). Akiwa hapo uwanja wa
ndege langoni alikuta teknolojia ya kisasa
kabisa, ambapo gari kuingia unabonyeza
mashine, bonyeee, inatema kadi ya kulipia
gharama za kuingia uwanjani hapo.
MN kwake ni kawaida kuingia Uwanja wa
Ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
Dar es Salaam upande wa Terminal II.
Teknolojia aliyoitaja napo ipo. Tena MN
anaangalia kwa jicho la furaha upande wa
Terminal III. Ingawa haijazinduliwa, lakini
parking zake zilivyopangiliwa zinavutia.
Sasa MN amepata mshituko wa mwaka.
Terminal I ni uwanja wa kihistoria. Uwanja huu
ni sura ya Tanzania, kwa maana kuwa watalii
wengi wanaotumia ndege ndogo wanatoka na
kuingilia katika Terminal I.
MN aliyoyaona Terminal I yanatisha. Kwanza ni
kwenye maegesho ya magari. Katika jengo la

Utawala Terminal I, MN ameona jambo la
kutisha. Yanapoegeshwa magari ya mabosi,
bati la banda linahatarisha maisha. Magari
yanaegeshwa chini ya bati lililooza, lenye kutu
ya mwaka, lakini mbao au vyuma
walivyoezekea vimekatika, limeinama.
Jinsi paa lilivyokaa na magari yakiwa
yanaendelea kuegeshwa chini yake, inatia doa
taifa letu. Inaharibu heshima na taswira ya nchi
yetu. Si kuharibu heshima tu, bali pia ni hatari
kwa watu wanaoingia kuegesha magari.
Siku ikitokea wakati mtu anaegesha gari
ukatokea upepo mkali, MN anaona taifa
litapoteza watu na magari. Kwa kweli MN
anasema yapo mambo ambayo hata kama
yanasubiri zabuni, basi kwa kulinda maisha ya
watu na heshima ya nchi, wahusika
wayakarabati kwa fedha za ndani.
MN kinachomshangaza ni kwamba hata kama
wakubwa wa uwanja huo wanasubiri bajeti ya
Serikali Kuu, inakuwaje wanashindwa kutumia
hiyo Sh 2,000 wanayotutoza kwa saa
kukarabati hata mashimo yaliyotamalaki katika
maegesho?
Kimsingi, MN anaona taifa letu linapata aibu
kubwa. MN anaona kuna watu waliouzoea huu
uchafu na maegesho yaliyochoka kwa kila hali

hapo Terminal I. MN anadhani wakati wa
kuwaondoa wahusika umefika ili waletwe watu
wenye fikra mpya, watakaokarabati maegesho
ya Terminal I ili kuepusha aibu hii.
MN anatoa onyo na kusema wakubwa hawa
wasiporekebisha paa la maegesho ya ofisi za
viongozi pale Terminal I na kukarabati mashimo
kwenye maegesho ya wateja wanaolipa Sh
2,000 yao kisha tairi za magari yao zinachanwa
na mashimo ya lami, hatasita kumwambia
mtumbuaji awatumbue bila soni. Chukueni
hatua.

Ends…

By Jamhuri