…Kutokana na tukio hilo Serikali ya Kenya
ilimuamuru mwanamuziki huyo mwenye
sauti nzito kuondoka mara moja nchini
humo kutokana na kutokubaliana na vitendo
vya udhalilishaji kwa wanawake.
Onyesho lililokuwa limepangwa kufanyika
lilifutwa, wapenzi na mashabiki wake
wakibaki wakisubiri kwa hamu.
Kama hiyo haitoshi, mwaka 2012, Olomide
alipatikana na hatia ya kumshambulia na
kumjeruhi msimamizi wake wa karibu,
Diego Lubaki, nchini Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo.
Katika shambulio hilo, Olomide alihukumiwa
kifungo cha miaka mitatu, lakini
hakukitumikia kifungo hicho gerezani baada
ya kulipa faini.

Inaelezwa kuwa mwanamuziki huyo
alimshambulia Lubaki kutokana na
mabishano baina yao kuhusu deni la dola
za Marekani 3,700.
Olomide anatajwa kuwa mwanamuziki
mwenye visa. Katika visa vyake aliwahi
kulighadhabisha Kanisa Katoliki
alipojiongezea jina la ‘Benedict wa 16 wa
Kongo’

, jina ambalo lilikuwa la Papa

Benedict wa 16 wakati huo.
Ni mwanamuziki mwenye mbwembwe
awapo jukwaani na mwenye kujituma
kiburudani.
Majina yake halisi anaitwa Antonie
Christophe Agbepa Mumba, aliyezaliwa
Julai 13, 1956 katika mji wa Kisangani,
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Olomide ana asili ya nchi mbili; Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Sierra
Leone.
Mama yake ni raia wa Kongo DRC, akitokea
katika kabila la Songye, ambalo
linapatikana Mkoa wa Kasai, wakati baba
yake ni mwenye asili ya nchi ya Sierra
Leone.

Kwa mujibu wa mila na utamaduni wa kabila
la babu zake, mama yake alimpa jina la
‘Koffi’ kutokana na kuzaliwa siku ya Ijumaa.
Akiwa bado ‘kinda’ Olomide alipachikwa jina
bandia la ‘Antoine Makila Mabe’

, likiwa na

maana ya ‘damu mbaya ya Anthony.’
Alianza safari ya muziki mwanzoni mwa
miaka ya 1970, katika bendi ya Viva la
Musica, iliyokuwa na wanamuziki wengi
magwiji akiwemo Papa Wemba.
Olomide alianza kazi katika bendi hiyo
akiwa mtunzi na mwandishi wa nyimbo na
baadaye aligeukia katika uimbaji.
Kama wahenga wasemavyo kuwa atafutaye
hachoki, akichoka ujue kesha pata. Mwaka
1986 alianzisha bendi iliyofahamika kwa
majina ya ‘Quartier Latin International’.
Baada ya miaka kadhaa kupita, bendi hiyo
ilijizolea umaarufu kimataifa hususan katika
Bara la Afrika na Ulaya, hivyo akawa na
mashabiki wengi.
Baadhi ya albamu zake zilizotoka ni ‘Tcha
Tcho’ ya mwaka 1990,

‘Haut da gamme’ ya

mwaka 1992,

‘Noblesse Oblige’ ya mwaka

1994 na ‘Magie’ ya mwaka 1995.
Zingine ni pamoja na ‘Gagi’ ya ‘Film Diva’
ya mwaka 1995,

‘V 12’ ya mwaka 1996,

‘Loi’ ya mwaka 1997,

‘Droit de Veto’ ya

1998,

‘Attent’ ya mwaka 1999,

‘Force de

frappe’ ya mwaka 2000,

‘Efrakata’ ya

mwaka 2001,

‘Affaire d’ Etat’ ya mwaka

2003,

‘Monde arabe’ ya mwaka 2004 na
‘Bord Ezang Kombo’ ya mwaka 2008.
Antoine Koffi Olomide alikulia katika familia
ya watu wenye uwezo wa kati na mahali
ambapo elimu ilikuwa ikipewa kipaumbele.
Olomide pamoja na kupenda muziki tangu
akiwa mtoto, ndoto zake kubwa zilikuwa
awe mchezaji wa mpira wa miguu.
Alipoanza kupevuka akiwa na umri wa
miaka 18, wakati huo, akiwa mwanafunzi
kijana, alivutiwa sana na usanii pamoja na
muziki, ndipo alipoanza kutunga na kuimba
nyimbo.
Kwa mujibu wa historia hiyo, Olomide
alikuwa na akili sana darasani, hali ambayo
ilimfanya apate wadhamini wa kumlipia
fedha kwenda kusoma mjini Bordeaux,
Ufaransa, ambapo alipata Shahada yake ya

kwanza ya Biashara na Uchumi.
Mbali na shahada hiyo, inaelezwa pia ana
shahada ya pili katika masuala ya Hisabati
kutoka Chuo Kikuu cha Paris, Ufaransa.
Akiwa Paris alianza kujifunza kupiga gitaa
na kuandika nyimbo, aliporudi DRC alijiunga
na bendi ya muziki ya Viva la Musica
ambayo ilikuwa ikiongozwa na Papa
Wemba.
Baada ya kujiunga na bendi hiyo, Olomide
aliimarisha mtindo wa polepole wa
‘Soukous’ uliokuwa umekwisha
umaarufu aliouita ‘Tcha Tcho’.
Baada ya miaka kumi ya mafanikio yake,
akatamani kuwa mwanamuziki wa
kimataifa. Ilipofika mwaka 1988 wimbo wa
‘Henriquet’ ukatokea kuwa mkali
uliosababisha kupachikwa jina bandia la
‘Golden Star’.
Koffi Olomide aliyafurahia mafanikio zaidi
baada ya kuandika wimbo akiwa na binti
yake pekee, Minou, ukiitwa D’elle et Moi’
miaka ya 1990.
Olomide tangu mwaka 1990 hadi 1994,
alifurahia kukua kwa mafanikio
yake ambayo kwa kipindi cha miaka chini ya

minne, alifyatua zaidi ya albamu saba
zikiwa chini ya jina lake na kundi lake la
‘Quartier Latin’.
Mwaka 1992 alichaguliwa kuwa mwimbaji
bora wa kiume na mshindi wa video bora
katika shindano la African Music Awards
mjini Abidjan, Ivory Coast.
Yaelezwa kwamba ujuzi wa aina yake na
mpangilio mzuri wa muziki vimempa
umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi
yake ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC).
Alifyatua albamu yake kali inayotamba ya
‘Abracadabra’

, iliyotanguliwa na albamu

za ‘Ngounda’
,
‘Efrakata’
,
‘Tcha Tcho’
,
‘Haute de Gamme – Koweit’ na ‘Rive
Gauche’.
Baadhi ya nyimbo za nguli huyu ni pamoja
na ‘Loi’
,
‘Magie’
,
‘Stila’
,
‘Sexy Pop’
,

‘Rounge A Levre’
,
‘Etant Civil’
,
‘Round

Poit’
,
‘San suit’
,
‘Respect 2’
,
‘l Autre la’
,

‘Miss Dess’
,
‘Nolesse Oblige’ na ‘Escola
Phamacien’. ‘Wimbo wa ‘Phamacien’
sehemu kubwa ya uimbaji ametamba
aliyekuwa mwimbaji wake Fally Ipupa.
Mwaka 1998, Olomide akiwa katika Jiji la

Paris nchini Ufaransa, alikimbiwa na
wanamuziki takriban wote, baada ya
onyesho kubwa lililofanyika katika Ukumbi
wa Olympia.
Bendi hiyo ilisambaratika na baadhi ya
wanamuziki wake wakaenda kuunda bendi
yao ya Orchestra ‘Quartier Latin Academia’.
Baada ya tukio hilo, Olomide hakuteteleka
kabisa, kwani haikuchukua kipindi kirefu
akawaibua tena vijana wengine wenye vipaji
kutoka sehemu mbalimbali nchini humo.
Amewafundisha wanamuziki wengi chipukizi
ambapo wengine wameamua kujitegemea
na kusimama wenyewe katika kazi za
muziki na wengine bado wapo na bendi hiyo
hiyo.
Baadhi ya wanamuziki ambao amekwisha
kuwatoa ni Fele Mudogo, Motana Kamenga,
ambaye alitimka kwenda kujiunga na bendi
ya Big Star ya General Defao.
Wengine ni pamoja na Bruno Mpela, Soleil
Wanga, Sam Tshintu, Suzuki 4 by 4, Ferre
Gola na Fally Ipupa.
Olomide aliwahi kufika hapa nchini mwezi
Desemba 2012 na kumwaga burudani
kabambe zilizokonga nyoyo za Watanzania

waliohudhuria onyesho lake lililofanyika
katika viwanja vya Leaders, Kinondoni
jijini Dar es Salaam.
Nyimbo zake mpya zinazotamba hivi sasa
ni ‘Tshou Tshou’
,
‘Nyataquance’
,
‘Selfie’
,

‘Mbirime’
,
‘Afrakata’
,
‘Charisma’
,
‘Salopette’
,

‘L’amour N’existe pas’
,
‘Diaspora’ na

‘Sixieme’.
Koffi Olomide ni baba wa familia ya mke na
watoto saba.
Julai 13, 2018 ametimiza miaka 62, huku
akiendelea na shughuli za muziki licha ya
misukosuko hiyo kumharibia kazi yake.
Olomide ametangaza kung’atuka kwenye
shughuli ya muziki baada ya kutoa albamu
yake mpya ambayo iko studio kwa sasa.
Hii itakuwa ni albamu ya 20 ya
mwanamuziki huyu ambaye anamaliza
akiwa na mafanikio na hadi sasa albamu
zake tatu zimeorodheshwa kwenye orodha
ya albamu 1,000.

Mwandishi wa makala hii anapatikana
kwa namba: 0784331200, 0767331200 na
0713331200.

Mwisho

By Jamhuri