KATAVI

Na Walter Mguluchuma

Ajenda ya ajira kwa watoto imekuwa ikisumbua vichwa vya wengi duniani na mara kwa mara hujadiliwa kwenye vikao vizito vya kitaifa na kimataifa.

Umoja wa Mataifa (UN) unapinga ajira kwa watoto na ipo mikataba na makubaliano kadhaa yamesainiwa, Tanzania pia imesaini kupinga ajira kwa watoto.

Je, tatizo hili ni kwa nchi maskini au ni uzembe wa viongozi? Tanzania ni miongoni mwa nchi maskini duniani? Mkoa wa Katavi nao ni miongoni mwa mikoa au maeneo maskini nchini?

Maswali haya yanahitaji utulivu mkubwa kuyapatia majawabu stahiki. Lakini ukweli ni kwamba, ajira kwa watoto inaendelea na ni suala la kawaida katika Manispaa ya Mpanda ambako ndiko makao makuu ya Mkoa wa Katavi.

Nikisema makao makuu ya mkoa maana yake ni kwamba viongozi wote wanaopaswa kumsaidia Rais wa Tanzania kutekeleza yale yaliyosainiwa kimataifa, wapo hapa. Kila siku.

Mji wa Mpanda, miongoni mwa miji mikongwe nchini, ni kawaida sana kuwaona watoto wenye umri mdogo wakizunguka mitaani kutembeza biashara hata nyakati za masomo!

Lakini zaidi biashara hizo za watoto huendelea hadi nyakati za usiku, hivyo kuhatarisha afya yao ya mwili na akili (saikoloji), mbali na kuhatarisha maisha yao kwa ujumla.

Ni tatizo kubwa sana na hakuna dalili ya kupatikana suluhu katika siku za karibuni.

Biashara zinazozungushwa mitaani na watoto hawa ni miwa, karanga, matango, ndizi, mahindi na sasa kubwa zaidi ni vyuma chakavu.

Hii ni aibu kwa mkoa lakini hasa kwa sisi wazazi na zaidi viongozi wenye jukumu la kusimamia sheria na kulinda haki za watoto.

Ipo mitaa mjini Mpanda ambayo kimaadili haifai kutembelewa na watoto. Hii ni Mtaa wa Simba na Mtaa wa Fisi. Mitaa hii kwa sasa ndiyo gumzo mjini kwa starehe.

Wakati serikali ikipamba na tatizo la mimba za utotoni, viongozi wa Katavi ni kama hawana habari na mapambano hayo ingawa ukweli ni kwamba mkoa huu ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa mimba za utotoni, ukiwa na asilimia 45 kitaifa. Aibu.

Swali kwa wazazi, walezi na hasa viongozi wa serikali; tatizo la mimba za utotoni litakwisha lini Katavi? Au tukubali tu kuishi nalo milele?

Viongozi, wazazi tumeshindwa kuwajibika? Tunaona sifa gani kuwa vinara wa upuuzi huu nchini? 

Ni wazi kwamba biashara zinazofanywa na watoto wanaopaswa kuwa shuleni ni moja ya vyanzo vya upuuzi huu.

Biashara hizi za kurandaranda wala hazifanywi kwa siri! Kila mtu anawaona watoto hawa wa kike na wa kiume, ingawa madhara yanatofautiana kijinsia.

Mimba ni madhara kwa watoto wa kike na mmoja wao amekiri mbele ya JAMHURI kutakwa kimapenzi na wanaume tofauti wengine wakiwa wenye umri mkubwa kuliko baba yake.

“Mimi siendi shule kwa kuwa wazazi wangu ndio wanaonituma kuja mjini kufanya biashara,” anasema binti mmoja ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Shanwe.

Anasema biashara hiyo ndiyo humpatia mahitaji ya shule (ambako haijulikani huwa anasoma lini au siku ngapi kwa muhula) na kwamba kwake: “Mimi naona ni jambo la kawaida tu. Hakuna aliyewahi kuniuliza kwa nini nipo mitaani nafanya biashara wakati wa masomo. Wewe (mwandishi wa JAMHURI) ndiye wa kwanza.” 

Mmoja wa wakazi wa mjini Mpanda, Juma Mnyema, anakiri kuwa hii ni aibu kwa manispaa na mkoa kwa ujumla.

Mnyema, mkazi wa Majengo, anasema tatizo hili ni bomu litakalokuja kulipuka siku za baadaye.

“Kuna wakati Mkuu wa Mkoa aliyeondoka amewahi kulivalia njuga suala hili na hali ikaanza kuwa shwari. Sioni kwa nini lisiwezekane sasa. Watoto lazima warejee madarasani,” anasema.

Kauli yake inaungwa mkono na Doto Sylvester, mkazi wa Rungwa, akisema biashara hizi ndizo chanzo cha utoro wa watoto shuleni na uharibifu wa miundombinu kutokana na wizi wa vyuma ambavyo watoto wa kiume huvisaka ili kwenda kuviuza kama vyuma chakavu.

“Viongozi na wazazi tumeshindwa kuwadhibiti watoto hawa. Hii si aibu tu, bali ni hatari kwa mkoa na taifa zima kwa ujumla,” anasema Sylvester.

Anasema iwapo mkoa umeshindwa kudhibiti, basi wakati umefika kwa viongozi wa kitaifa kuliingilia na kuleta suluhu ya kudumu.

Miongoni mwa madhara ya watoto kuanza kuzurura mitaani na kujitafutia riziki ni kuibuka kwa vikundi vya kuhalifu vinavyohusisha watoto wenye umri kati ya miaka 11 na 15.

Vikundi hivi vinavyojiita ‘manyigu’ na ‘damu chafu’, vimeutikisa Mji wa Mpanda kwa miezi kadhaa vikifanya uporaji na kujeruhi watu nyakati za usiku kwa kutumia mapanga na marungu.

Hawa, kwa mujibu wa uchunguzi wa JAMHURI, ni watoto wenye wazazi wao mkoani hapa wala hawajatoka nje ya nchi au nje ya mkoa.

Ni watoto waliozaliwa na wazazi wakazi wa Nsemulwa, Kawajense, Kashaulili, Mpanda Hotel na kwingineko.

Ndiyo. Ni watoto wadogo kabisa wenye umri wa chini ya miaka 16. 

Hili limedhihirika majuzi baada ya Jeshi la Polisi kufanya msako mkali na kuwakamata watoto zaidi ya 30 wanachama wa ‘manyigu’ na ‘damu chafu’.

Ni watoto wanaoishi mitaani mwetu; yaani tunaishi nao Makanyagio, Mpanda Hotel na Nsemulwa; wanafahamika lakini polisi hawapewi ushirikiano katika harakati zao za kudhibiti uhalifu huu kwa wazazi na majirani kuficha taarifa.

Na sasa kuna kila dalili ya kuibuka kwa wimbi kubwa la watoto wa mitaani ambalo halijawahi konekana mjini Mpanda.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Ali Makame Hamad mara kwa mara amekuwa akisema kuwa wamekuwa wakifanya jitihada za kukabiliana na vikundi hivyo kwa kuwapatia elimu wazazi wa watoto hao na wananchi juu ya madhara ambayo yanaweza kutokea endapo wataendelea kuwakumbatia wahalifu pasipo kutoa taarifa polisi.

Walau watoto 11 waliokamatwa wamekwisha kufikishwa mahakamani.

Lakini juhudi hizo za polisi peke yao hazitoshi kumaliza tatizo kubwa linaloonekana.

0784 909 721

By Jamhuri