Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Geita

JESHI la Polisi mkoani Geita linamtafuta mchimbaji wa madini ya dhahabu Mashaka Jeremia kwa tuhuma za kumchoma mkewe visu sehemu mbalimbali ya mwili wake na kusababisha kupoteza maisha .

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ally Kitumbu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema chanzo ni mgogoro wa kifamilia kati ya marehemu na mumewe.

Kamanda amesema kuwa baada ya mume wa marehemu Amina Hassan kufanya uhalifu huo alitoroka.Kamanda amesema kuwa Polisi wanaendelea na jitihada za kumtafuta mtuhumiwa huyo.

Mganga mfawidhi hospitali ya Mkoa wa Geita, Dkt.Mfaume Salum amethibitisha kutokea kwa kifo hicho ambapo amesema Agosti 31, 2022 saa sita usiku walimpokea marehemu Amina akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake yaliyosababishwa na kitu chenye ncha kali.

Amesema marehemu alikuwa na majeraha maeneo ya mgongoni, kifuani na tumboni yaliyoleta madhara kwenye viungo vilivyoko ndani ya tumbo na kifuani na kufanyiwa upasuaji usiku huohuo na na alipotoka kwenye chumba cha upasuaji alipoteza maisha.

“Mama huyu baada ya kupokelewa alikua ana majeraha sehemu za mwili hasa tumboni na tulibaini yameleta madhara katika viungo vilivyoko ndani ya tumbo tulimfanyia upasuaji usiku huo huo na baada ya kutoka kwenye chumba cha upasuaji baada ya masaa 20 alifariki,” amesema Dkt. Salum.

Mtoto wa marehemu (jina linahifadhiwa) ambaye nu mwanafunzi wa shule ya sekondari Mujumuzi amesema alishuhudia, ambapo wazazi wake walikua wakigombana usiku na baba yake kuanza kumpiga kisha kutoa kisu kwenye mfuko na kuanza kumchoma mama yake na kumsababishia majeraha makubwa.

Amesema wakati baba yake akiendea kumchoma kisu mama yake alifungua dirisha kuomba msaada ndipo baba alipomuacha na kufungua mlango kisha kukimbia.

By Jamhuri