nmb-4Nianze kwa kuwashukuru makumi ya wasomaji ambao wameendelea kununua nakala ya kitabu changu kipya kiitwacho, ‘Mfanikio ni haki yako’. Kitabu hiki kinauzwa kwa njia ya mtandao, ambako ukishalipia fedha unatumiwa kwa njia ya barua pepe. 

Kitabu hiki kinauzwa Sh. 5,000 tu, kimo katika mfumo wa PDF, hivyo unaweza kukisoma hata kupitia simu yako ya kiganjani. Nimeamua kwenda na teknolojia ili kuwafikia wengi kimaarifa. Kama hujapata nakala yako, wasiliana nami mapema, uungane na walioamua kufanikiwa.

Leo nitachambua kuhusu nafasi ya wataalamu katika biashara zetu. Nakumbuka nikiwa chuo kikuu nimewahi kuingia kwenye mgogoro wa kimtazamo na wahadhiri wangu. Mtazamo huu ulikuwa “Ni kwanini wanafundisha vitu ambavyo hawajavithibitisha kwa vitendo?”

Mtazamo na msimamo wangu huu ulisababisha kupishana na wahadhiri wangu wakati nikisoma chuo kikuu, shahada ya kwanza ya usimamizi na utawala wa masuala ya biashara. Sikuwa na ugomvi katika masomo mengine isipokuwa katika masomo mawili ambayo kwa muono wangu, yamebeba kiini cha shahada hiyo. 

Somo la kwanza lilikuwa ni la ujasiriamali (Entrepreneurship, Small Business Management & International Entrepreneurship) na jingine lilikuwa ni uanzishaji na usimamizi wa miradi (Projects Planning and Management). 

Kabla hawajaanza kunifundisha nilitaka kufahamu sifa walizonazo katika maeneo hayo. Wa ujasiriamali nilitegemea kuona kuwa ni mfanyabiashara mkubwa na yule wa miradi nilitegemea kuona kuwa ni mmiliki wa miradi halisi iliyofanikiwa sana. 

Kwa bahati mbaya hawakuwa na sifa nilizozitazamia (uzoefu wa vitendo katika maeneo hayo), badala yake walikuwa ni wasomi wenye shahada nyingi na sifa zinazong’ara katika vyeti vyao, wenyewe wanaitaCV.

Nakiri wazi kuwa pamoja na kusoma masomo hayo, lakini walionifundisha (yaani wahadhiri wangu) hawakuweka hamasa yeyote katika fikra zangu kuhusu ufanyaji ujasiriamali na uendeshaji wa miradi.

Hadi leo huwa nawahesabu kama watu wanaofundisha vitu ambavyo wao wenyewe vimewashinda! Ni bahati kuwa nilikuwa nikisoma masomo hayo huku nikiwa tayari nina nguvu na hamasiko binafsi moyoni mwangu la kufanikiwa sana katika miradi na ujasiriamali. Hii ndiyo iliyokuwa salama yangu.

Ndio maana kila siku ninapojiuliza ni kwa nini tunazalisha wasomi wengi wenye vyeti katika maarifa ya biashara, lakini hatuoni wakitumia elimu zao kuibua miradi, biashara na kutengeneza ajira; ninabaini kuwa moja kwa moja tatizo lipo kwenye mifumo yetu ya kielimu.

Ni vigumu sana kwa daktari ama profesa wa biashara (ambaye hana hata banda la chipsi tu) kuzalisha mfanyabiashara halisi. Anachoweza kufanya ni kuzalisha wenye vyeti wengi ambao wanabaki kuwa mizigomitaani.

Kama ambavyo huwezi kujifunza kuogelea kwa kusoma maandishi, pia haiwezekani kujifunza biashara kwa kusoma vitabuni pekee.

Kama inavyotakiwa kuingia majini na kuanza kugusa maji, ndivyo ilivyo hata kwa biashara, ni lazima uingie na kuionja. Mkufunzi wa uogeleaji atafanikiwa kuzalisha waogeleaji wengi na walio mahiri kwa kuonesha kwa vitendo namna ya kuogelea (ikiwamo upigaji mikono na urushaji miguu awapo majini). 

Mkufunzi akikaa ukingoni mwa bwawa na kuwasomea wanafunzi maandishi kisha kuwaamuru wajitose majini, anaweza asishuhudie hata mmoja anayejitosa. Lakini hata wakijitosa majini na wakapata tatizo la kuanza kuzama, huyu mkufunzi atawasaidiaje kuwaokoa wakati yeye mwenyewe hayajui maji? 

Ndivyo ilivyo pia kwa wasomi wakufunzi wa mambo ya biashara na ujasiriamali. Hatuwezi kuzalisha wajasiriamali wa‘ukweli’ ikiwa wanaowafundisha hawajawa mifano ya kuigwa (they are not role models). Hali hii tete inaibua tatizo jingine kubwa katika ujasiriamali wa kitanzania pale zinapohitajika huduma za kitaalamu ikiwemo ushauri wa kibiashara.

Kiukweli ushauri wa kitaalamu katika ujasiriamali na biashara unahitajika sana hasa katika nyakati hizi ambazo tunapambana na ushindani wa kimataifa. Unaposikia neno ushauri pamoja na mantiki yake ni kwamba huwa una machaguo matatu.

Unaweza kuukataa wote, unaweza kuutumia wote ama ukachukua kidogo na kuikataa sehemu fulani. Yote katika yote ushauri wa kibiashara tunatazamia unapotumika ulete tija ya uboreshaji wa biashara ama eneo uliloshauriwa.

Tanzania hii asilimia kubwa ya wafanyabiashara wanalalamikakwa kutozwa kodi kubwa kuliko inavyostahili kutokana na ukosefu wa elimu katika eneo hilo.

Kwa kukosekana mifumo ya utunzaji wa mahesabu, Mamlaka ya Mapato (TRA) huamua kukadiria viwango vya kodi bila kuzingatia faida inayokusanywa kwa mwaka. Angalia mfano huu mdogo; unapokuwa na duka lako, kabla ya kulipa kodi unatakiwa kutoa mshahara wako (wewe mjasiriamali) mshahara wa wafanyakazi pamoja na gharama za uendeshaji. 

Baada ya pale ndipo unapotakiwa kulipa kodi kutoka katika kile kinachobaki. Lakini ni wangapi wanafanya hivyo? Bila shaka utagundua kuwa ni wachache mno. Habari njema ni kuwa huhitaji kuwa msomi ili kuendesha biashara zako kisomi, watumie wasomi wakusaidie kufikia malengo yako (lakini nakushauri utumie aina ya wasomi ninaowaamini mimi-wale wanaoishi kwa vitendo maarifa yao).

Kwa mfano; kama wewe ni mfanyabiashara wa huduma za daladala ama unakusudia kuanzisha biashara hiyo, ni vema ukamtafuta mfanyabiashara mzoefu katika eneo hilo la daladala ili akupe ‘specific’ mbinu na mazingira halisi. Huyu kwako mimi ninamhesabu ni mtaalamu wako. Itakuwa ni bahati tu inapotokea umeniomba ushauri wa kibiashara halafu ikawa kuwa biashara unazofanya ama kukusudia kufanya ni zile ambazo mimi pia  ninazifanya.

Maana yangu hapa ni kuwa utaalamu katika biashara upo wa aina mbili. Kuna wale waliokaa darasani na kufundishwa biashara (bila kujali ikiwa wanafanya ama hawafanyi biashara) na wengine ni wale ambao licha ya kutoingia darasani, wana uzoefu mkubwa wa kibiashara.

Hawa wote ni vema kuwatumia kwa kadiri ya mazingira na mahitaji yako kibiashara (japokuwa mimi huwa siwatumii hata kidogo wasomi wa biashara wanaozijua nadharia na hawajawahi kuzitumia katika mazingira halisi ya kibiashara)

Unapotafuta mtaalamu wa kukushauri (ikiwa unataka msomi) mimi ninadhani ni vema kuwapata wataalamu ambao wana uzoefu wa kivitendo katika biashara mbalimbali.

Najua hii ni changamoto kubwa kwa sababu wasomi wengi wa mambo ya biashara hawafanyi biashara, lakini kwa kuwa tunao wasomi wachache wa biashara ambao wanafanya biashara ni vema kuwatumia hao. Bila kuwa makini unaweza kupotezwa kwa sababu ‘wataalamuwengi hutumia muda mwingi kueleza namna mambo yasivyowezekana.

Hata hivyo, katika ufanyaji biashara, ni vema sana kuachana na mazoea ya kufanya biashara kienyeji, badala yake kuna umuhimu wa kuingiza utaalamu katika ujasiriamali wetu. Hii itasaidia sana kuratibu mafanikio yako na kuachana na hesabu za kubahatisha kwa kwenda kwa kupapasa.Tunapaswa kuwatumia wataalamu washindi katika biashara zetu.

By Jamhuri