Hivi karibuni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alipowasilisha hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka fedha 2015/16 mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alizungumzia mambo mengi ambayo ni muhimu kwa mdau au mmiliki yeyote wa ardhi kuyafahamu.
Kati ya mambo muhimu aliyozungumza, mawili yaligusa hisia za wengi. Kwanza ni punguzo katika kodi, ada na tozo za ardhi. Pili ni suluhu kuhusu suala la muda mrefu la uendelezaji wa mji mpya wa kisasa wa Kigamboni.
Yumkini, Mji wa Kigamboni ni suala lililokuwa likisubiriwa kwa hamu hasa kutokana na sintofahamu na danadana kwa muda mrefu. Makala hii itaeleza baadhi ya mambo muhimu kutoka hotuba ya Serikali kuhusu mambo mbalimbali ya ardhi awamu kwa awamu.
Tutazungumzia kuhusu kodi, tozo na ada zilizopunguzwa ili watu wafahamu, hasa kutokana na ukweli kuwa ni wachache ambao hufuatilia hotuba hizi. Na baadaye makala zitakazofuata siku nyingine zitaeleza msimamo wa Serikali kuhusu ardhi ya Kigamboni.

Ada, Kodi na tozo zilizopunguzwa
(i) Punguzo la ada ya upimaji

Kwa kawaida mtu anapohitaji hati huwa ni lazima eneo lako liwe limepimwa. Upimaji ni hatua ya awali kabisa unapohitaji hati. Hata hivyo, hatua hii huwa ni lazima kwa wale wenye maeneo ambayo hayajapimwa kabisa.
Aidha, ifahamike kuwa suala la kupima ardhi si lazima tu uwe unahitaji hati bali waweza kupima eneo lako kama hatua ya kurasimisha (officialise) eneo lako ili litambuliwe katika mamlaka za ardhi.
Ada ya kupima iliyokuwapo ilikuwa ni Sh 800,000 (laki nane tu) kwa hekta. Imepungua mpaka kufikia Sh 300,000 (laki tatu) kwa hekta. Ni punguzo la asilimia 62.5. Ni punguzo kubwa, lakini kwa misingi ya umiliki ardhi hata hiyo bado ni kubwa. Ikumbukwe kuwa ardhi inayoongelewa hapa haihusishi mashamba. Ni ardhi ya kawaida ya makazi au viwanja.

(ii) Punguzo la kodi ya upimaji mashamba ya biashara
Kwa kawaida, mashamba ya biashara hulipiwa kodi tofauti na mashamba ya kawaida katika upimaji. Kwa hiyo, kodi hii hapa ni kwa ajili ya kupima mashamba ya biashara tu. Awali, kodi hiyo ilikuwa Sh 10,000 (elfu kumi) kwa ekari. Na sasa ni Sh 5,000 (elfu tano) kwa ekari. Ni punguzo la asilimia 50.

(iii) Punguzo la kodi upimaji mashamba ya kawaida
Mashamba ya kawaida ni mashamba ambayo si ya biashara. Ni mashamba ambayo ndiyo yanayomilikiwa na Watanzania kwa asilimia kubwa. Takribani wakulima wote tunaowasikia huko mikoani humiliki mashamba ya namna hiyo.
Awali kodi ya upimaji kwa ekari ilikuwa Sh 1,000 (elfu moja) na sasa ni Sh 400 (mia nne) kwa  ekari. Ni punguzo la asilimia 60.

(iv) Punguzo gharama za kuweka vizuizi (caveat)
 “Caveat” ni kizuizi ambacho huwekwa na yeyote mwenye maslahi fulani katika ardhi ili kuzuia hati isibadilishwe kutoka kwa mmiliki mmoja kwenda kwa mwingine pengine kutokana na mauzo au mkopo.
Kizuizi hiki hakiwekwi mahakamani isipokuwa huwekwa na mamlaka za ardhi. Ada ya kuweka kizuizi awali ilikuwa Sh 120,000 (laki moja na elfu ishirini), na sasa ni Sh 40,000 (elfu arobaini).  Ni punguzo la asilimia 66.7.

(v) Punguzo nyaraka za ubadilishaji majina (Deed poll)
Deed Poll ni waraka maalum ambao hutumika endapo mtu anataka kubadilisha jina. Kwa mfano, mtu anaitwa AUDAX lakini amebadilisha jina na sasa anaitwa PETER, basi nyaraka ya kisheria inayotumika huitwa deed poll.
Serikali iliuweka waraka huu kwenye mamlaka za ardhi na hushughulikiwa na mamlaka hizo. Ada iliyokuwa inalipiwa awali ni Sh 80,000 (elfu themanini tu) na sasa ni Sh 30,000 (elfu thelathini tu). Ni punguzo la asilimia 62.5.

(vi) Punguzo gharama za kupata nakala ya hukumu katika mabaraza ya ardhi (Mahakama za Ardhi).
Mabaraza ya ardhi ndiyo Mahakama za Ardhi. Yapo ya Mabaraza ya Ardhi ya Kata na baadaye Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya ambayo ndiyo Mahakama za Ardhi za Wilaya.
Ili kupata nakala ya hukumu kesi inapoisha, muhitaji hutakiwa kulipia. Awali malipo ya nakala hizo ilikuwa Sh 16,000 (elfu kumi na sita tu), na sasa ni Sh 6,000 (elfu sita tu). Ni punguzo la asilimia 62.5.

(vii) Punguzo ada ya maombi ya kumiliki ardhi
Mara nyingi maombi haya hufanyika iwapo kuna ardhi mahali isiyokuwa na mmiliki au ardhi iliyo katika mamlaka za serikali na sasa serikali inataka kuwamilikisha wananchi. Hapa ndipo hutakiwa kufanyika haya maombi.
Awali ada ya maombi kama haya ilikuwa Sh 80,000 (elfu themanini), na sasa ni Sh 20,000 (elfu ishirini tu). Ni punguzo la asilimia 75. Tutaendelea kuwaletea mapunguzo mengine katka makala zijazo. Aidha, ni vema kuzingatia kuwa mapunguzo haya yataanza kutumika rasmi Julai mosi, 2015.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, ndoa kampuni n.k tembelea:
sheriayakub.blogspot.com

 

By Jamhuri