Wingi wa watu: Athari, faida zake

Uzazi wa mpango umekosolewa na baadhi ya watu kuwa ni njama za nchi za Magharibi ambazo zinakabiliwa na tatizo la, ama kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa, au kuwa na familia ambazo hazina watoto kabisa.
Kwa upande mmoja wingi wa watu ni suala linaloweza kuipa nchi nguvu dhidi ya nchi nyingine. Kwa mantiki hiyo, kushawishi nchi zinazoendelea kupunguza kasi ya kuzaliana kumeonekana kama ni njama ya kupunguza nguvu hii inayotokana na idadi kubwa ya watu.
Hakuna ubishi kuwa kuna nguvu kubwa ambayo inatokana na wingi wa watu ingawa ni dhahiri pia kuwa kuna namna nyingi za kupima nguvu hii. Iwapo tunazungumzia juu ya watu wengi walioelimika, ambao wanaishi maisha ya neema na afya njema, na ambao wana pesa za kukidhi mahitaji yao, basi tunaweza kusema kuwa nguvu hiyo inaweza kupimwa kutokana na manufaa ya kiuchumi ambayo yatajitokeza kwenye nchi wanayoishi.


Idadi kubwa ya watu inabeba sura mbili; inaweza kuwa ni tatizo kwa nchi, lakini inaweza kuwa chanzo cha kuletea nchi manufaa.
Eneo moja ambako nchi inaweza kuathirika kwa kuwa na idadi kubwa ya watu ni pale inaposhindwa kuzalisha chakula kutosheleza mahitaji ya watu waliopo. Nchi yenye idadi kubwa ya watu na ambayo haizalishi chakula cha kutosha italazimika kutumia rasilimali zilizopo kununua chakula cha kuwalisha watu wake. Italazimika kupunguza matumizi kwenye huduma muhimu za jamii na kufidia pengo la chakula kitakachohitajika.


Uamuzi mgumu utaikabili nchi kama kuamua kununua chakula kwanza, na dawa baadaye. Au hata kuwepo vipindi ambako haitawezekana kununua dawa za kutosha.
 Ipo hatari ya kuwa na idadi kubwa ya wananchi ambao ni masikini wanaotegemea misaada ya wengine, au ya serikali, na ambao hawana uwezo wa kuchangia chochote kwenye maendeleo ya nchi. Wanabaki kuwa mzigo mkubwa kwa nchi, pamoja na kwa wale wachache wenye kipato cha uhakika.
Kwenye nyumba ambayo mzazi mmoja tu anafanya kazi familia nzima inamtegemea huyo mmoja. Anapofanya kazi mzazi wa pili inawezekana kushirikiana kukabiliana na jukumu la kutunza familia na kupunguza mzigo kwa mzazi mmoja pekee. Utaongezeka uwezekano kuwa kiasi kikubwa zaidi cha pesa kitaingia benki kuliko kile kitakachotoka.


Njia moja inayofahamika ya kutumia idadi kubwa ya watu kama kitegauchumi kwa nchi ni kwa serikali kupanga mikakati ya kutoa elimu bora kwa raia wake. Uboreshwaji wa kiwango cha stadi za watu sambamba na kuwapo kwa ajira na shughuli nyingine zinazoongeza kipato kutawezesha watu kuboresha maisha yao, kulipa kodi na kuitajirisha Mamlaka ya Mapato Tanzania. Badala ya kuwa mzigo kwa jamii raia anakuwa msaada kwa jamii, kama ambavyo mzazi wa pili anapopata ajira na kupunguza mzigo wa kutunza familia.
 Kwenye ulimwengu huu wa utandawazi raia ambaye hana elimu anajipunguzia uwezo na nafasi ya kushinda changamoto zinazomkabili. Aliyesoma anayo nafasi kidogo. Nafasi hiyo inapopatikana, au kupitia ajira au kwa kujiajiri mwenyewe, basi anaongezeka mtu mmoja zaidi ambaye analeta faida kwa jamii badala ya kuwa mzigo.


Wadau wote wa maendeleo, ikiwa ni pamoja na serikali, sekta binafsi, na vyuo vya mafunzo, wanapaswa kumulika ili kubaini fursa na changamoto zilizo mbele yetu kama taifa kwa madhumuni ya kuweka mikakati inayoandaa mitaala itakayokidhi mahitaji ya sasa, ya muda mfupi, na ya muda mrefu ya wahitimu ili kuoanisha rasilimali watu na mahitaji ya ajira na shughuli za kibiashara na kiuchumi.
Yapaswa kujifunza kutoka kwa baadhi ya nchi kama India ambayo inao wanasayansi na watafiti 454 kwa kila watu milioni moja wanaounda kundi la waajiriwa. Huu ni mfano mmojawapo wa kuwekeza kwenye aina ya elimu ambayo inaweza kuwa kichocheo kikubwa kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Kampuni za kimataifa hufanya jitihada kubwa ya kutafuta nchi zenye nguvu kazi iliyoelimika ili wahamishie viwanda kwenye nchi hizo kwa ajili ya kupata unafuu wa gharama za uzalishaji. Ni hatua ambayo Uchina imepitia na ambayo imeleta manufaa makubwa katika sekta ya biashara na uchumi. Ni hatua ambayo nchi yetu inaweza kupitia iwapo itajiandaa vyema.


Ipo hatari ya kuigeuza nchi inayoendelea kuwa soko kubwa la ajira kwa nchi zilizoendelea bila kuleta manufaa makubwa, lakini zipo tahadhari za kisera na kisheria ambazo zinaweza kuandaliwa kuhakikisha kuwa manufaa hayo yanapatikana na yanaonekana kwa wananchi na siyo kwenye takwimu za uchumi tu.
 Ipo mifano hai hapa hapa Tanzania ya msingi wa kujenga kada ya raia wenye elimu nzuri. Nitatoa mfano wa kisiwa cha Ukerewe ambako niliarifiwa miaka karibu 10 iliyopita ilikuwa na karibu watu 70 wenye elimu ya ngazi ya shahada ya uzamivu. Yawezekana hiyo idadi imeshavuka 100 sasa hivi.
Labda hoja siyo ukubwa wa idadi ya watu kwenye nchi. Hoja ya msingi ni kuwapo kwa wingi wa watu wa aina gani? Wenye elimu ya kiwango gani? Na wanaochangia kiasi gani kwenye maendeleo ya nchi yao? Wengi wanaweza kuwa faida kwa nchi yao kama wameandaliwa vizuri kielimu na zipo fursa kwao za kupata ajira na shughuli za kuongeza kipato.
Pamoja na kutafakari mambo mengine, tunatumaini wale wanaotaka kurithi kazi ya Rais Jakaya Kikwete wanakoswa usingizi kutafuta majibu ya maswali haya.