Kangi LugolaMgonjwa afikapo kwa tabibu – iwe wa kienyeji, tiba za asili au wa kisasa – hakurupukiwi kupewa dawa.
  Mtaalamu wetu wa jadi atapiga ramli kubaini chanzo cha kuumwa na upande wa yule wa tiba za kisasa atautanguliza uwezo wake mkubwa wa kusikiliza vyema kwa muktadha wa kiitwacho ‘doctor-patient relationship’ ili kuweza kumtibu mgonjwa wake bila mawaa.
Nimeanza na maneno haya katika kule kubainisha matatizo lukuki na kutafuta mujarabu wake wa dhati kama wafanyavyo wataalamu wetu walioiva kutibu.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alinukuliwa akisema, “Hatuna budi hasa katika majadiliano na mazungumzo yanayohusu Jumuiya, tujifunze kusikiliza hoja zilizotolewa na wenzetu na kuzijibu kwa kuzikubali au kuzikataa, bila kujali kama aliyezitoa ni rafiki au si rafiki,” mwisho wa nukuu.
Ukiifuatilia kwa karibu, mingi ya mijadala ya kwenye vijiwe vyetu vya kahawa na hata ile rasmi, hutosita kung’amua kuwa wengi wetu huwa na hulka ya kutosikiliza kwa kujenga bali ubishani wa mashindano yasiyokwisha, humo wapo wachache wanaopenda kujifunza kwa kubeba ujumbe waliopewa na kuufanyia kazi kitunduizi!


Kangi Lugola, Mbunge wa Mwibara (CCM), ni mmoja wa wabunge wachache ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wenye tabia ya kuzungumza kwa mifano bayana.
Ukiweka hisia hasi pembeni, utautanabahi uwezo wake mkubwa wa kujieleza na kuchambua mambo kwa kueleweka kirahisi hata na vijana wadogo wa umri wa kupevuka.
Mbunge huyu ananikumbusha mwalimu wangu wa kemia sekondari ya juu, ninayemkumbuka kwa jina la Wambali maarufu ‘So much simple’ kama jina linavyojieleza.
Wale wote waliopitia masomo ya ziada kipindi yamepamba moto jijini Dar es Salaam katika shule za Makongo, Pugu, Minaki, Azania, Green Acres, Jangwani na hata Kibaha na Mzumbe wanamfahamu sana mwalimu huyu kwa kuhanikiza semi fasaha za Kiswahili, ucheshi wake, utani na vituko vya kila namna wakati wa ufundishaji wake na alivyo gwiji utamwelewa utake usitake hata kwa wale walio wazito sana kujifunza.


Nimekuwa nikiwasikia wanaomjua Kangi Lugola kuwa ana tabia ya “kufundisha” kwa viitwavyo vituko, leo sitaviongelea vyote bali vichache na vya karibuni.
Liko lile tukio la kuchangia hoja nzito akiwa amejifunika ‘soksi’ usoni akitaka kusikilizwa kwa umakini, huku akisema kuwa anataka kumuua nyani na hawezi kumwangalia usoni kwa kuchelea kujaa huruma naye!
Ukirejea hili la majuzi wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Serikali kuhusu kushuka kwa thamani ya shilingi yetu, mzalendo huyu aliingia ndani ya ukumbi wa Bunge akiwa na ‘fuko’ lililojaa bidhaa mbalimbali na kuanza kuchangia kwa kusema, “Mheshimiwa Spika nina bidhaa hapa ambazo hata hazistahili na hizi ndizo zinazoshusha shilingi yetu.


“Nimekuja na kontena zima, kama ingewezekana kuingia nalo hapa ningeingia nalo, humu kuna soksi kutoka Marekani, dodoki za plastiki, leso, chaki, nyembe, pamba za kusafisha masikio, vijiti vya kuondoa mabaki ya chakula, rula na penseli – vyote kutoka China na pipi kutoka Kenya.”
Ni ukweli wa mambo kuwa Serikali inajitahidi kupambana dhidi ya ujinga, maradhi na umaskini lakini ni lazima twende mbele na kuzidi kuiongeza kasi hiyo kwa kubuni njia bora zaidi kuliko tulizo nazo sasa.
Wakati Edward Lowassa akitangaza ‘Safari ya Matumaini’, alikaririwa akisema kuwa endapo atapitishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea wake wa urais, atakitanguliza kipaumbele chake  cha elimu, akikipa nguvu kwa kumrejea Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair, kuwa pamoja na taifa lao kupiga hatua kubwa ya maendeleo ya sayansi, teknolojia na viwanda, alipoulizwa kipaumbele chake alirudia mara tatu, ‘Kipaumbele cha kwanza “ELIMU”; cha pili “ELIMU” na cha tatu “ELIMU”.
Ni kwanini basi nimegusia suala la elimu ilhali makala yangu inajikita katika hoja ya Kangi Lugola na kushuka kwa thamani ya shilingi yetu?


Jibu rahisi ni kuwa tunapoamua kuwa na dhamira ya dhati ya kulifanya bora taifa letu pendwa katika tasnia ya uchumi, hatutashangaza na kuchekwa eti kwa kutaka kuithubutisha vyema elimu yetu iendane na kasi ya uchumi wa Ujamaa na Kujitegemea, iendane na kasi ya soko huria na pia kasi ya soko jamii.
Bilionea wa Marekani, Bill Gates, aliwahi kuishauri Afrika na nchi zinazoendelea juu ya kuichora upya elimu yetu iendane na mazingira tuliyo nayo, na pia soko letu hasa la ndani na pia la nje.


Katika hili hili, wamepatikana wakosoaji wazalendo wakiitoa kasoro elimu yetu na ithibati zitolewazo na Kamisheni ya Elimu ya Juu (TCU) katika kuanzisha utitiri wa vyuo vikuu nchini.
Ikumbukwe kuwa unapokuwa na wingi wa vyuo vikuu, ni lazima pia uwe na soko la ajira kwa wahitimu, vinginevyo zitaendelezwa zile kauli nyepesi zinazochosha, “eti vijana hawajiajiri” na wala “si wabunifu.”
Ni kweli wako waliokosa elimu ya kujiajiri, lakini hata wale waliyonayo hupata mikingamo kutokana na upatikanaji mgumu na masharti mazito ya mikopo!


Wakosoaji hao wanakwenda mbali kwa kusema kuwa tunahitaji uwepo wa vyuo vingi vya kati, vyuo hivyo vya ufundi vitazalisha wataalamu wengi wenye uwezo wa ubunifu na uzalishaji utakaoendana na soko – liwe la ndani na nje, kinyume chake, kusuasua kwa kada hiyo kunasababisha kupatikana wataalamu wachache wasioendana na soko la ushindani, na hata wale wachache huzalisha bidhaa chache zisizohimili nguvu ya ‘mafuriko’ ya bidhaa za nje na hapa ndipo ilipo sintofahamu anayoitafutia tiba Lowassa ndani ya safari yake ya matumaini na aliyoigusia Lugola bungeni.
Katika hilo, ni hivi karibuni Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa David Msuya, alikaririwa akiihusisha elimu ‘isiyoshiba’ na kushuka kwa thamani ya shilingi yetu, naye akitambaa kwa kule kutozalisha vyema na kutosafirisha bidhaa zetu huku Taifa likiwa ‘gulio’ la bidhaa zilizo na zisizo na ubora kutoka nje ya nchi.
Hatuna budi kuzisikiliza kwa utulivu na kuzielewa hoja za watangaza nia wa urais wa CCM, hasa wanaotanguliza elimu yetu wakiwa na lengo la kuiimarisha na kuifanya bora kuliko ilivyo sasa, na ni imani yangu hata ilani ya uchaguzi wa chama iliyoandaliwa chini ya Stephen Wasira itakuwa imeithubutisha ukweli wa kuthubutika!


Ukarimu huanzia nyumbani na ‘inajuzu’ kabla ya kuutoa nje, basi hatuna budi kujiimarisha na kuwa bora hasa kielimu na kiuchumi, ili tuzidi pia kuwa na sera bora za uhusiano ya kimataifa.
Lugola hakukosea, mifano na vituko vyake vimeeleweka na vinaendelea kueleweka na wote wanaoipenda Tanzania na kutaka iwe bora zaidi kivitendo.
Hakika binadamu wote ni sawa na kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.
 
0714-534574, akyala@live.com

 
2668 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!