Juzi jioni, mtoto wangu wa mwisho nilisikia anataka kugombea udiwani uchaguzi ujao, nikamuuliza maswali machache na aliweza kuyajibu kwa ufasaha.
 Nikajua kweli huyu mtoto kawa mwanasiasa mkomavu katika umri mdogo. Nilipomuuliza sababu za kutokugombea katika uchaguzi uliopita, alijitetea kuwa umri wake ulikuwa haujatimia.
Wakati wa maisha yetu ya siasa ya Ujamaa na Kujitegemea masuala ya uongozi yalikuwa ni karama na uwezo wa mtu, hayakuwa masuala ya kukurupuka kama mwanangu na kudai kuwa anaweza. Lakini pia masuala ya uongozi enzi zetu yalikuwa ni masuala ya maadili bora katika jamii na kukubalika kwa busara na hekima ya mgombea.


Sina hakika na hali ya sasa katika siasa za hapa nyumbani au nchi zilizoendelea kama Tanzania yetu, ninachoweza kusema ni mabadiliko ya kimfumo wa kiuongozi katika nchi yetu, hivi sasa baada ya kuacha mfumo wa siasa yetu tuna namna nyingine ya mfumo ambao kamwe kwa umri wangu siwezi kuuzungumzia.
Siasa yetu ndiyo ninayoweza kuizungumzia, siasa ya mtu kuwa mwadilifu katika matendo yake, siasa ya kiongozi kuwa mfano kama ilivyokuwa kwa Julius enzi zetu, siasa za kujitolea badala ya siasa za kulipwa, siasa ya kuombwa kugombea na siyo kuomba kugombea, siasa ya umaskini wa fedha na utajiri wa kujitolea na siyo siasa ya ukwasi wa fedha na kuwa sehemu ya ajira.


Ninachoweza kusema ni aina ya siasa ya mgombea kuwa lazima awe maarufu na siyo makini kama ilivyokuwa enzi zetu. Na haya ni mabadiliko ambayo hatuna budi kuyapokea kama wananchi ambao kwa uzuzu na kwa maoni yetu tunaona kuwa ndiyo mfumo bora kuliko ule tuliokuwa tunautumia.
Napenda siasa, lakini nachukia aina ya siasa yetu, ni lazima niwe mkweli na kwamba mbomoko huu tunautengeneza wenyewe kutokana na ujinga wetu, mwaka fulani nakumbuka enzi zile za Julius kuna mgombea mmoja maarufu sana aliyejishughulisha na sanaa aliwahi kukataliwa katika vikao halali na makini vya TANU juu ya uanasiasa wake wa umaarufu.


Hakuna shaka kuwa sasa ni tofauti na zamani na kiwango cha elimu kimeongezeka miongoni mwa Watanzania, lakini shaka yangu ni pale ambako kila  mtu anapoweza kusema anaweza pasi na kujua hali tuliyonayo au wapi tunatakiwa kwenda hasa katika kipindi hiki cha sayansi na teknolojia.
Kwa wale ambao wana muda kama wangu wa kufuatilia mijadala mingi ya siasa kama mimi, watakuwa ni miongoni mwa wagonjwa wenzangu wa kichwa kwa yale ambayo wanayasikia, mathalani kama unafuatilia mijadala ya Bunge utaona jinsi ambavyo kiti cha Spika kinavyokuwa na kazi ngumu ya kuongoza Bunge.
Kama unamuangalia na kumsikiliza mwanasiasa katika jukwaa na kama ni mwanasiasa majitaka inabidi uwe na aspro ya kutuliza maumivu ya kichwa, hii yote inatokana na uwezo wa wanasiasa wetu ambao wengi wao hawakidhi mahitaji ya viwango vyetu vya siasa ya enzi zetu.
Leo nimeamua kuandika waraka huu kutoa angalizo kwa wapiga kura wenzangu kujiuliza maswali kadhaa kabla ya kushika kalamu na kuchagua kiongozi mwanasiasa, yapo maswali mengi lakini maswali machache ya kijinga ni vema yakawa haya:


Huyu ninayemchagua ana uwezo gani kielimu, na elimu yake ina uhusiano gani na nafasi ya uongozi? Huyu ninayemchagua kwanini anataka nafasi hii? Je, ni msaidizi wa wananchi au ni mganga njaa? Kwanini aombe nafasi hii? Sifa zake katika jamii ni zipi?
Tunajua kuwa hili ni kimbilio la wajanja wengi, lakini ni rahisi kuwatambua kwa kutambua michango yao ya mawazo kwa jamii inayowazunguka, na tufanye nini kujitoa katika vichwa vya hao wanasiasa? Je, fedha tutakazopokea kama rushwa na takrima zitatufikisha wapi baada ya kuwapa uongozi kwa miaka mitano.
Waswahili wanasema, “akili mu mkichwa,” mimi nimeshachoka kazi kwenu wapigakura maana sasa uwanja umevamiwa kila mtu ni mwanasiasa kisa anajulikana. Wachawi wa maendeleo ni sisi wenyewe, na acha tuendelee kujiloga zaidi Oktoba.
 
Wasaalamu
Mzee Zuzu
Kipatimo.

 

By Jamhuri