Na. Joseph Mahumi, WF, Dar es Salaam

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Czech zimetia saini Mkataba wa Kuondoa Utozaji Kodi ya Mapato Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji Kodi, hatua itakayosaidia kufungua uchumi wa nchi kwa kuvutia uwekezaji wa kimataifa na utawezesha wawekezaji na wafanyabiashara wanaofanya shughuli kati ya Tanzania na Czech.


Mkataba huo ujulikanao kama Agreement on the Avoidance of Double Taxation and Prevention of Fiscal Avoidance and Evasion in Respect to Tax on Income, umesainiwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), kwa niaba ya Tanzania, na Balozi wa Jamhuri ya Czech nchini Tanzania mwenye makazi yake ya kudumu nchini Kenya, Mhe. Nicol Adamcová, kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Czech, katika hafla iliyofanyika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alisema kuwa mkataba huo utasaidia kuondoa hatari ya kipato kilekile kutozwa kodi mara mbili katika nchi mbili tofauti, kuhamasisha sera za haki za kikodi, na kuimarisha imani ya wawekezaji.

“Mkataba huu ni hatua muhimu katika jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kufungua uchumi wa nchi kwa kuvutia uwekezaji wa kimataifa na utawezesha wawekezaji na wafanyabiashara wanaofanya shughuli kati ya Tanzania na Czech” alisema Dkt. Nchemba.

Aliongeza kuwa Takwimu za Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) zinaonesha kuwa nchi zilizo na mikataba madhubuti ya kuepusha kodi ya maradufu huvutia hadi asilimia 30 zaidi ya uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje, ikilinganishwa na zile zisizo na mikataba hiyo.

“kupitia Mkataba huu tunatarajia kuvutia mitaji mikubwa kutoka Czech kuja kuwekeza Tanzania, hususan katika sekta za kutengeneza magari na ndege, vifaa vya umeme, mitambo na mashine mbalimbali na kupitia uwekezaji huo, Tanzania inatarajia kunufaika na ukuaji wa sekta za uzalishaji, maendeleo ya viwanda, na kuongezeka kwa ajira kwa wananchi” alisema Mhe. Dkt. Nchemba.

Kwa upande wake Balozi wa Jamhuri ya Czech nchini Tanzania mwenye makazi yake nchini Kenya, Mhe. Nicol Adamcová, alisema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Czech ni wa muda mrefu na wenye tija, hivyo kusainiwa kwa mkataba huo utawapa fursa kwa wawekezaji wa Kitanzania kuwekeza nchini Czech bila vizuizi vya kikodi.

“Nina furaha kubwa kuwa tumetia saini mkataba huu na ni jambo muhimu, ni kipengele cha msingi kinachoonyesha kuwa kuna kiwango cha juu cha kuaminiana kati ya nchi zetu mbili, kama isingekuwa hivyo, tusingetumia muda na nguvu kujadiliana kuhusu” alisema Mhe. Adamcová.

Aliongeza kuwa makubaliano hayo ni muhimu na ni ushahidi muhimu wa utulivu wa mazingira na hali ya biashara katika nchi hizi mbili.

Kwa mujibu wa takwimu za UN COMTRADE, mwaka 2022 biashara baina ya Tanzania na Czech ilifikia takribani dola milioni 16.2 za Kimarekani, hasa katika sekta za mitambo, vifaa vya umeme, teknolojia za usafirishaji, na bidhaa za kilimo. Mkataba huu unatarajiwa kuongeza zaidi kiwango cha biashara na uwekezaji kati ya pande hizo mbili.