Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la kwanza lililoandaliwa na Taasisi ya Wasambazaji wa sekta ya Madini Tanzania (TAMISA) litakalofanyika Mei 16, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 14, 2025, Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano na Masoko TAMISA, Dkt. Sebastian Ndege amesema lengo la kongamano hilo ni kuangazia kuhusu nafasi ya Watanzania katika utoaji wa huduma kwenye sekta ya Madini.

Amesema kuwa, uzinduzi huo pia utaenda sambamba na uzinduzi wa Kamati Maalumu ya kutoa taarifa mbalimbali kuhusu uwekezaji kwenye sekta hiyo.
“Mei 16, mwaka huu TAMISA tunatarajia kuwa na kongamano kubwa ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mavunde ambapo pia ataambatana na viongozi wengine kutoka wizarani,” amesema.
Amesema TAMISA imejipanga kuwa na makongamano ya mara kwa mara ili kuweza kuwaweka pamoja wadau wa sekta hiyo ealiopo nchini na kukumbushana fursa zilizopo
“Mpaka sasa TAMISA ina wanachama zaidi ya 50 ambapo wamekidhi vigexo kwa kuzingatia ukubea wa Uwekezaji huo na tunawaomba Wadau wengine wa sekta hiyo kuona umuhimu wa kujiunga ili kubadlishana uxoefu na kutambuana zaidi.

“Tunawasihi watanzania wenye makampuni yanayotoa huduma katika sekta hiyo kujiunga na TAMISA ili kupata taarifa mbalimbali zinazohusu sekta hiyo,” amesema Dkt Ndege
Naye Mwenyekiti wa TAMISA, Peter Kumalilwa amesema lengo la kuanzishwa kwa TAMISA kuwa ni pamoja na kuboresha maudhui ya ndani, kuimarisha mazingira ya biashara kukuza utamaduni wa uvumbuzina ushirikiano Kati ya wadau na uendelevu wa biashara ndani ya mfumo wa maudhui.

“Sisi kama TAMISA, ni sauti ya watoa zuduma wengine wote ambao ni wazawa, tunajaribu kuona ni kwa namna gani ambavyo wananufaika na Sh. Trilioni 3.1 ambazo zinatumika katika manunuzi migodini,” amesema Kumalilwa.
Amefafanua kuwa, taasisi hiyo imedhamiria kuwajengea Watanzania uwepo ili waweze kunufaika zaidi na utoaji huduma zinazohitajika, hatua ambayo itapunguza malalamiko kuwa wageni wananufaika kupitia fursa hizo migodini.
