Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP-CENTRE), David Kafulila, amesema kasi kubwa ya ongezeko la watu nchini ni miongoni mwa changamoto zinazoathiri ukuaji wa uchumi na kiwango cha kipato cha mtu mmoja mmoja.
Akizungumza katika mhadhara wa Umma uliofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) leo (Jumatano, Juni 3, 2026), Kafulila amesema Tanzania ina wastani wa ongezeko la watu unaozidi asilimia 3 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, kiwango hicho ni kikubwa kuliko wastani wa bara la Afrika wa asilimia 2 na wastani wa dunia wa asilimia 1 kwa mwaka.
Amesema ongezeko hilo kubwa la watu lina athari katika mgawanyo wa matokeo ya ukuaji wa uchumi kwa wananchi, kwani ukubwa wa uchumi unapogawanywa kwa idadi kubwa ya watu, kiwango cha kipato cha mtu mmoja mmoja hupungua.
“Kasi yetu ya ongezeko la watu ni changamoto katika uchumi wetu. Tunaongezeka kwa kasi zaidi kuliko wastani wa Afrika, jambo ambalo linaathiri kiwango cha kipato cha mtu mmoja mmoja,” amesema Kafulila.
Kafulila pia amegusia mjadala unaoendelea kuhusu athari za ongezeko la watu katika uchumi, akikiri idadi kubwa ya watu si tatizo moja kwa moja ikiwa watu hao watakuwa na uwezo wa kuchangia uzalishaji na maendeleo.
“Watu wanaweza kuongezeka na kuongeza uchumi, lakini pia wanaweza kuwa mzigo kwa uchumi. Kuna watu ambao ni rasilimali na kuna ambao ni mzigo. Kazi ya vyuo vikuu ni kuwabadilisha watu kutoka kuwa mzigo kwenda kuwa rasilimali,” amesema.


