Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Dar es Salaam

Watanzania wameaswa kuwa makini na baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), wanaharakati na wanasiasa wanaodaiwa kutumia fedha kutoka mataifa ya nje kuhamasisha vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani, umoja na mshikamano wa taifa.

Rai hiyo imetolewa leo Juni 4, 2026 jijini Dar es Salaam na mwanafalsafa wa Pan-Afrika kutoka Zimbabwe, Dk. Joshua Maponga, wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa makala inayochambua matukio yaliyojitokeza kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, pamoja na hali ya sasa na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha matukio hayo hayajirudii.

Dk. Maponga aliwataka Watanzania kuendelea kulinda sifa ya nchi yao kama “Kisiwa cha Amani” kwa kuepuka kushawishiwa na watu wanaotumia mitandao ya kijamii au majukwaa mbalimbali kuchochea vurugu na migawanyiko.

“Watanzania ni mfano wa kuigwa barani Afrika kwa kudumisha amani. Nawasihi msiwasikilize wanaharakati na wanasiasa wanaochochea vurugu na uvunjifu wa amani kwa sababu hawana nia njema kwa taifa hili,” alisema Dk. Maponga.

Aliongeza kuwa Serikali inapaswa kufanya uhakiki wa kina wa baadhi ya mashirika ya kiraia ili kubaini vyanzo vya fedha wanazopokea na namna zinavyotumika, akieleza kuwa baadhi yao wanaweza kuwa tishio kwa ustawi na usalama wa taifa iwapo hawatasimamiwa ipasavyo.

Kwa mujibu wa Dk. Maponga, watu wanaochochea vurugu mara nyingi huishi nje ya nchi katika mazingira salama, huku wananchi wanaoshiriki machafuko wakibeba gharama kubwa ikiwemo kupoteza maisha, mali na makazi yao.

Aidha, amewataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kwa kuwapa wananchi elimu kuhusu madhara ya vurugu na maandamano yasiyo ya amani, akisema kuwa matukio hayo yanaweza kudhoofisha maendeleo na kuathiri rasilimali za taifa.

Makala hiyo imeandaliwa na kampuni ya African Spear Head Media kwa lengo la kuchambua matukio yaliyotokea kabla na baada ya uchaguzi pamoja na athari zake kwa maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa African Spear Head Media, David Hundeyin, alisema Tanzania ni moja ya nchi muhimu kiuchumi barani Afrika kutokana na nafasi yake ya kimkakati, hususan kupitia Bandari ya Dar es Salaam ambayo hutumiwa na mataifa mbalimbali katika shughuli za biashara na usafirishaji.

Alisema wananchi wanapaswa kuendelea kulinda amani na rasilimali za nchi yao kwa kuwa machafuko yanaweza kusababisha kuyumba kwa uchumi na kuathiri maendeleo ya taifa.

“Vurugu na mauaji yaliyotokea Oktoba 29, 2025 yalikuwa na athari kubwa kwa jamii. Hata hivyo bado kuna baadhi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuhamasisha vurugu. Wananchi wanapaswa kuwa makini na watu wa aina hiyo kwa sababu hawana nia njema kwa taifa lao,” alisema Hundeyin.

Alisisitiza kuwa amani, umoja na utulivu ni nguzo muhimu za maendeleo endelevu, hivyo kila Mtanzania ana wajibu wa kushiriki katika kuvilinda na kuvienzi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.