Na Mwandishi wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Tanzania imeendelea kuonyesha mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa (AMR), baada ya kupunguza matumizi ya dawa za antibiotiki kwa asilimia 88 na kupunguza vifo vinavyohusishwa na tatizo hilo kwa asilimia 14.
Mafanikio hayo yamebainishwa wakati wa Kongamano la 17 la Uwasilishaji wa Matokeo ya Tafiti la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), ambapo wataalamu walieleza kuwa licha ya hatua zilizofikiwa, maambukizi yanayosababishwa na vimelea sugu kwa dawa bado ni tishio kubwa kwa afya ya umma, usalama wa chakula na maendeleo ya uchumi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Juni 2026, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Uratibu wa Sekta Mbalimbali kuhusu Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa (MCC), Profesa Hezron Nonga, alisema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Kitaifa wa Kudhibiti Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa wa mwaka 2023 hadi 2028, unaotekelezwa kwa kutumia mfumo wa “Afya Moja” unaounganisha afya ya binadamu, mifugo na mazingira.
Profesa Nonga alisema Tanzania imepiga hatua kubwa kutoka katika hali ya kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na tatizo hilo mwaka 2016 hadi kufikia mwaka 2024 ambapo imejenga mifumo imara ya udhibiti na ufuatiliaji wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa.
Alisema serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa, kuboresha ushirikishanaji wa taarifa, kuongeza fedha za ndani kwa ajili ya mapambano dhidi ya AMR na kuendesha kampeni mbalimbali za uelimishaji wa umma kuhusu matumizi sahihi ya antibiotiki.
“Usugu wa vimelea dhidi ya dawa unatishia kufuta mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya kwa miongo kadhaa. Ni muhimu kuendelea kuwekeza katika tafiti, ufuatiliaji na matumizi sahihi ya dawa ili kuhifadhi ufanisi wa dawa zinazookoa maisha,” alisema Profesa Nonga.
Kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, tatizo la AMR linahusishwa na vifo vya takribani watu milioni 4.71 kila mwaka duniani, huku zaidi ya watu milioni 1.14 wakifariki moja kwa moja kutokana na maambukizi yanayosababishwa na bakteria sugu kwa dawa.
Profesa Nonga alisema Tanzania imeongeza juhudi za kutoa elimu kwa umma kupitia kampeni ya “Holela Holela Itakukosti” pamoja na kuanzisha istilahi ya Kiswahili ya “Usugu wa Vimelea vya Magonjwa Dhidi ya Dawa (UVIDA).”
Alisema kampeni hiyo imewafikia karibu watu milioni 25 na kutambuliwa na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC).
Aidha, alisema uzingatiaji wa kanuni za kinga na udhibiti wa maambukizi katika vituo vya afya umeongezeka kwa asilimia 60, huku maboresho katika chanjo za mifugo, usalama wa mifugo na usalama wa chakula yakichangia kupunguza milipuko ya magonjwa na matumizi yasiyo ya lazima ya dawa kwa wanyama.
Kwa upande wake, Mkuu wa Ushirikiano wa Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Luc Blanco, alisema usugu wa vimelea dhidi ya dawa ni miongoni mwa vitisho vikubwa vya afya ya umma duniani na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto hiyo.
Alisema mapambano dhidi ya AMR yanahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali na mataifa mbalimbali, huku tafiti, ufuatiliaji na kubadilishana taarifa vikibaki kuwa nyenzo muhimu za kufanikisha juhudi hizo.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Erasto Mbugi, akizungumza kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Appolinary Kamuhabwa, alisema vyuo vikuu vina nafasi muhimu katika kuzalisha ushahidi wa kisayansi unaosaidia kutunga sera na kuimarisha uwezo wa taifa kukabiliana na changamoto mpya za afya.
Kongamano hilo liliwakutanisha watafiti, watunga sera, wataalamu wa afya na wadau wa maendeleo chini ya kaulimbiu isemayo: “Kuimarisha Mapambano dhidi ya Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa nchini Tanzania: Tathmini ya Mafanikio, Changamoto na Mwelekeo wa Baadaye kwa Mtazamo wa Afya Moja.”





