Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imewasilisha mpango wake wa makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ukilenga kuimarisha ajira staha kwa vijana na wanawake kupitia Programu ya Building a Better Tomorrow (BBT) pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kilimo na miundombinu ya umwagiliaji.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Wizara yake imepanga kukusanya jumla ya Shilingi 12.26 bilioni kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato ambapo Shilingi 8.66 bilioni zitatokana na ukaguzi wa mazao, kodi za majengo na uuzaji wa nyaraka za zabuni, huku Shilingi 3.6 bilioni zikipatikana kupitia ada za umwagiliaji na ukodishaji wa mitambo.

Akizungumza Bungeni leo Mei 21,2025 Jijini Dodoma, Waziri Bashe ameomba Bunge liidhinishe matumizi ya jumla ya Shilingi trilioni 1.24 kwa mwaka huo wa fedha.
Kuhusu miradi ya Maendeleo na Matumizi ya Kawaida, Wizara imeomba Shilingi bilioni 838.26, ambapo Shilingi bilioni 702.28 zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo, zikiwemo Shilingi bilioni 424.33 kutoka vyanzo vya ndani na Shilingi bilioni 277.95 kutoka nje.
Fedha nyingine ni Shilingi bilioni 135.98 zitatumika kwa matumizi ya kawaida, ikiwa ni pamoja na Shilingi bilioni 81.45 kwa mishahara ya watumishi na Shilingi bilioni 54.54 kwa matumizi mengine ya wizara, bodi na taasisi zake.

Waziri Bashe amesema Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaomba kuidhinishiwa Shilingi bilioni 382.14, kati ya hizo Shilingi bilioni 308.72 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo (zikiwemo Shilingi bilioni 259.62 kutoka ndani na Shilingi bilioni 49.10 kutoka nje), na Shilingi bilioni 73.42 kwa matumizi ya kawaida ambapo Shilingi bilioni 8.27 ni kwa ajili ya mishahara na Shilingi bilioni 65.15 kwa matumizi mengineyo.
Kuhusu Tume ya Maendeleo ya Ushirika, jumla ya Shilingi bilioni 22.58 zinaombwa, ambapo Shilingi bilioni 21.88 ni kwa matumizi ya kawaida (mishahara Shilingi bilioni 12.85, matumizi mengineyo Shilingi bilioni 9.03) na Shilingi milioni 697.18 kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa fedha za ndani.
Kwa upande mwingine Waziri huyo mwenye dhamana ya Kilimo amesema Ajira kwa Vijana na Wanawake Kwenye Mashamba Makubwa Mbali na makadirio ya fedha, Serikali imeeleza maendeleo ya utekelezaji wa Programu ya BBT inayolenga kuimarisha ajira za vijana na wanawake kupitia miradi mitano.
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na mashamba ya pamoja, mitaji, huduma za ugani, uongezaji thamani wa mazao, na umwagiliaji,Shamba la Chinangali (ekari 1,772) limekabidhiwa kwa vijana 261 na linaendelea kuzalisha mazao mbalimbali.

Aidha, shamba la Ndogowe (ekari 11,453) limekabidhiwa kwa vijana 342, huku miundombinu muhimu ikiwa tayari imejengwa.
Aidha ameutaja mradi mwingine mkubwa ni Shamba la Mapogoro mkoani Mbeya ambalo litafadhiliwa kwa Dola milioni 129 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika, ikiwa ni hatua ya kukuza kilimo kikubwa chenye tija nchini.
