KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ali ussi amewataka wakandarasi waliopewa kazi za miradi ya kimkakati ya maendeleo kuitekeleza kwa viwango vyenye ubora hatua ambayo inalenga kujibu changamoto za wananchi.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa uwekaji wa Jiwe la Msingi katika mradi wa ujenzi wa Shule ya Amani katika eneo la Makuyuni wilayani Korogwe.

Alisema serikali imewekeza fedha nyingi kwenye miradi hiyo hivyo ni vizuri ikajengwa kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha hizo.
Aidha, amewataka wakandarasi hao kukamilisha miradi hiyo kwa wakati hususani kama ambavyo ilivyotarajiwa Ili iweze kuwanufaisha wananchi wa maeneo husika.

“Niwaombe ndugu zangu wakandarasi Mwenge wa Uhuru umeridhishwa na kazi hii mliyofanya katika hii shule lakini hakikisheni kazi zilizobaki zinamaliza kwa wakati Ili mradi huu uweze kutumika na kuleta matokeo tarajiwa Kwa watumiaji wake,”amesema kiongozi huyo.
Hata hivyo, Mbunge wa Jimbo la Korogwe vijijini, Timotheo Mnzava alimshukuru Rais Samia kwa kuwapelekea mradi huo wa shule ya amali ambao utaweza kuleta tija ya ujuzi na ufundi kwa vijana wao
Awali akitoa taarifa ya mradi huo Mkurungenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Good luck Mwangomango alisema kuwa mradi huo umegharimu zaidi ya Sh milioni 584 na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu.
