π Azindua maduka ya kisasa 31 Ushirombo
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewaasa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Bukombe wasikubali kuvutana na kugombana bali wadumishe amani, kuendelea kuheshimiana na kulinda utu wao hususan katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.
Dkt. Biteko amesema hayo Juni 14, 2025 wilayani Bukombe, mkoani Geita mara baada ya kuzindua maduka 31 ya kisasa yaliyopo katika eneo la Ofisi za CCM wilayani humo.
βNaomba niwakumbushe tena kwa sasa tunaukaribia mwezi wa Oktoba, 2025. Tunakaribia kuingia katika zoezi la Uchanguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, niwaombe tu kwamba, zoezi la uchaguzi ni zoezi la mara moja, lakini maisha yetu sisi yanadumu na yataendelea kudumu na kuna maisha baada ya kampeni na baada ya Uchanguzi. Hivyo, kwa heshima, nawaomba tuendelee kudumisha umoja, upendo na undugu uliopo baina yetu,β amesema Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine, amezungumzia ujenzi wa maduka hayo ya kisasa kuwa ni hatua kubwa kwa maendeleo ya wananchi wa eneo hilo la Ushirombo na maeneo mengine ya jirani kwa kuwa ni chanzo cha maendeleo na mzunguko wa fedha katika eneo hilo.
Amesisitiza β Maduka haya yataongeza mvuto na hivyo kuongeza thamani ya eneo hili la ardhi pamoja na thamani ya jengo. Ukuaji wa eneo letu hili huchangiwa zaidi na shughuli za madini na shughuli nyingine za kiuchumi. Taarifa zinaonesha kuwa, Mkoa wa Geita umeonesha kasi kubwa zaidi ya ukuaji kutokana na shughuli za madini, na watu wanaochimba watapata huduma kwenye hili,β
Aidha, amewapongeza na kuwashukuru Mwenyekiti na Katibu wa CCM Wilaya ya Bukombe na Madiwani 23 kwa ushirikiano wao na kusema kuwa wamefanya kazi kubwa ya kuchangia ujenzi wa maduka hayo na kusema kuwa anafurahishwa kufanya kazi nao akiongeza kuwa wajumbe wa kata wanazotoka wanaweza kuwapima kwa kazi walizofanya.

Dkt. Biteko amesema kuwa CCM katika wilaya hiyo itaendelea kuunga mkono mawazo mapya yatakayotolewa kwa ajili ya kusaidia maendeleo ambapo ametaja baadhi ya miradi ya ujenzi wa soko, stendi na barabara inayoendelea kujengwa wilayani humo inalenga kukuza uchumi wa wilaya na mkoa kwa ujumla.
Vilevile, Dkt. Biteko awaomba wanachama wa CCM kumuunga mkono kwa kumchagua Rais Samia na mgombea mwenza Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Geita, Nicholous Kasendamila amewapongeza CCM Wilaya ya Bukombe kwa ujenzi wa maduka hayo na kusema kuwa hilo ni darasa na siasa ni uchumi na ni wajibu wa CCM kukiimarisha chama chao.
Naye, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa, Mkoa wa Geita, Evarist Gervas amepongeza Dkt. Biteko kwa kuimarisha Chama katika wilaya hiyo na kushirikiana vizuri na viongozi wa Chama kwa kuimarisha wilaya hiyo kiuchumi.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa maduka hayo ya kisasa, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Bukombe, Leonard Mwakalukwa amesema kuwa Wilaya hiyo inatimiza sera ya CCM ya miradi ya uwekezaji na kwa kutambua kauli mbiu ya siasa na uchumi, ilitekeleza wazo la ujenzi wa maboresho ya vibanda hivyo 21 vilivyokuwepo awali liliasisiwa na Mbunge wa jimbo la Bukombe Dkt. Biteko.
Amesema Dkt. Biteko alitoa wito wa kuwa na vitega uchumi zaidi vya Chama cha Mapinduzi na kutunza na kuboresha mandhari ya eneo la CCM la Wilaya ya Bukombe. Ndipo Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Bukombe ikapitisha pendekezo hilo.
Ametaja faida za mradi kuwa ni pamoja na CCM wilayani humo kukusanya mapato kwa wingi.



