Na Allan Kitwe, Kasulu
SERIKALI ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepeleka zaidi ya sh bil 40 katika Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji safi na salama ili kumaliza kero ya wananchi.
Katika maeneo mengi ya Wilaya hiyo ikiwemo Kasulu Mjini huduma ya maji safi na salama imekuwa hairidhishi hali iliyopelekea kuwepo malalamiko ya mara kwa mara juu ya ubora wa maji yanayopatikana.
Akiongea na Mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake jana, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kasulu Mjini (KUWSSA) Nuru William Bagowe ameipongeza serikali kwa kusikia kilio cha wananchi.
Amesema kuwa katika kipindi cha miaka 5 tangu aingie madarakani, Rais Samia ameleta neema kubwa kwa wakazi wa Wilaya hiyo kwa kupeleka mabilioni ya fedha ambayo yamesaidia sana kutatua kero ya maji katika maeneo mengi.
Amebainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022, 2022/2023 na 2023/2024 miradi mikubwa ya maji yenye thamani ya zaidi ya sh bil 40 imetekelezwa katika Wilaya hiyo na kuboresha kwa kiasi kikubwa upatikanaji huduma ya maji safi.
Bagowe ametaja miradi hiyo kuwa ni ule wa Miji 28 ambao unagharimu kiasi cha sh bil 35 ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 45 na unatarajiwa kuhudumia wakazi wa kata 12 kati ya kata zote 15 zilizopo katika Halmashauri ya Mji Kasulu.
Mwingine ni ujenzi wa machujio ya Mto Chai na Miseno unaogharimu sh mil 385.5 ambao upo katika hatua za ukamilishaji na mradi wa maji Kidyama unaojengwa kwa ufadhili wa Shirika la Enabel kwa gharama ya sh bil 1.8.
Mradi mwingine mkubwa unaotekelezwa na serikali ya awamu ya 6 katika Wilaya hiyo ni uboreshaji huduma ya maji katika Mitaa ya Kabanga, Kimobwa, Mwilavya, Nyachijima, Nyarumanga, Kidyama na Kigondo unaogharimu bil 3.2.
Aidha katika kuhakikisha mfumo wa maji safi na maji taka unaboreshwa katika Wilaya hiyo, Bagowe alisema kuwa Rais Samia amewapatika kiasi cha sh bil 2.2 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa mfumo wa maji safi na maji taka.
Bagowe alimshukuru Rais kwa kuwapatia kiasi cha sh mil 497.5 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mpya ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kasulu Mjini (KUWSSA) ujenzi wake sasa umefikia asilimia 70 na kazi inaendelea vizuri.
