Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam,

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini imeanza rasmi zoezi la ukaguzi wa ubora wa malori yanaingia bandarini kwa ajili ya kushusha na kupakia mizigo inayopita katika Bandari ya Dar es Salaaam.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye bandari ya Dar es Salaam baada ya uzinduzi huo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mbossa, Naibu Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Baraka Mdima amesema kuwa Mamlaka imejipanga kutekeleza zoezi hilo kikamilifu na litakuwa ni endelevu.

“zoezi hili lina lengo la kuimarisha usalama wa watu, miundombinu pamoja na kuboresha utoaji huduma bora katika bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma,” alisema Dkt. Mdima.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania Dkt. Baraka Mdima (wapili kulia) akikata utepe wakati wa uzinduzi wa oparesheni ya ukaguzi wa malori yanayoingia kushusha na kupakia shehena katika bandari ya Dar es Salaam itakayoongozwa na kikosi cha Jeshi la Polisi kwa niaba ya TPA, wakwanza kulia ni Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed Gallus waliobaki ni maofisa wa Jeshi la Polisi Kituo cha bandari iliyofanyika jana.

Aidha, Dkt. Mdima aliwataka wamiliki na madereva wa malori hayo kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa na mamlaka yanatekelezwa ili kuondoa usumbufu unaoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo.

“Tunawataka wahusika kuhakikisha wanaleta malori yanayokidhi viwango vya ubora na ili kuepusha usumbufu, madereva wameelekezwa kuzingatia kuwa na leseni sahihi, vifaa vya kinga (PPE’s) na nyaraka nyingine husika”, alisema Dkt. Mdima.

Naibu Mkurugenzi huyo, pia aliwataka wamiliki na madereva ma malori hayo kuzingatia ubora wa matairi, mifumo imara ya breki, uwepo wa taa za tahadhari pamoja na kuhakikisha malori yote yanayoingia bandarini yana milango imara ili kurahisisha utoaji huduma yawapo bandarini.

Naye Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abed Gallus amesema kuwa wamekuwa na mazungumzo ya muda mrefu na Jeshi la Polisi yaliyojikita kuleta suluhu ya usalama na ufanisi wa uhudumiaji wa shehena bandarini.

Kwa mujibu wa Bw. Gallus hiyo yote ni katika kuhakikisha kuwa shehena zilizopo bandarini hapo inatoka na kuwafikia wateja kwa wakati na hatimaye kuifanya bandari kuwa shindani.

“Ili kuhakikisha tunaendelea na kasi ya uhudumiaji tuliyojiwekea, imetubidi kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha tunadhibiti malori mabovu yanayoingia kuchukua au kupakia mizigo bandarini,” alisema Bw. Gallus.

Maofisa wa Jeshi la Polisi kutoka kituo cha bandari ya Dar es Salaam wakiwa kwenye utekelezaji wa oparesheni ya kukagua malori yanayoingia kushusha na kupakia shehena katika bandari ya Dar es Salaam iliyofanyika jana.

Aidha, aliongeza kuwa zoezi ni sehemu ya maboresho makubwa yanayoendelea kutekelezwa bandarini ili kuongeza kasi ya uhudumiaji shehena inayopita katika bandari ya Dar es Salaam.

Alisema kuwa uwekezaji uliofanyika katika bandari ya Dar es Salaam umeongeza tija na ufanisi unaoendana na kasi ya uwekezaji, hivyo uwepo wa malori yasiyo na vigezo yatapelekea kukwamisha shughuli za kiutendaji bandarini.

Katika zoezi hilo lilizinduliwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, lilihudhuriwa pia Menejimenti ya TPA, pamoja na Jeshi la Polisi kituo cha Bandari ya Dar es Salaam.